Beled-weyne 3 Guri-el 2

Timu za Beled-weyne na Guri-el
Image caption Wasomali waanza kufurahia tena mechi za soka

Maeneo ya kati ya Somalia yameanza kufurahia soka, huku uongozi wa Al-Shabaab ukiendelea kudidimia.

Wachezaji soka wa timu ya wilaya ya Beled-weyne katika eneo la Hiiraan, waliweza kuifunga timu ya wilaya ya Guri-el magoli 3-2 katika mechi ya kirafiki iliyochezewa Guri-el, eneo la Galgadud, mwishoni mwa wiki.

Image caption Timu moja kusafiri hadi sehemu nyingine ni jambo linalowezekana sasa

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu kwa vijana kutoka eneo la Hiiraan kuweza kusafiri na kuingia eneo jirani la Galgaduud.

Eneo la Hiiraan limekuwa likisimamiwa na kundi la Al-Shabaab ambalo limekuwa likisaidiwa na Al-Qaeda, na soka ilipigwa marufuku katika eneo lote wakati kundi hilo likidhibiti sehemu hiyo.

Hayo yalikwisha wakati uongozi wa kundi hilo la Kiislamu ulipokomeshwa mapema mwaka huu.

Image caption Maeneo ya Somalia yameanza kucheza soka kutokana na uongozi wa Al-Shabaab kufifia

Mchezo huo wa kirafiki wa Guri-el uliochezwa tarehe 5 ulisimamiwa na Ali Hassan Beile na vijana wengine waliokuwa waamuzi, na waliopata mafunzo mwezi jana kutoka kwa chama cha soka cha Somalia.

Mwenyekiti wa kamati ya soka ya Galgadud, Abdirashid Aden Roble, akiikaribisha timu kutoka eneo la Hiiraan, aliwaelezea waandishi wa habari kwamba walifurahia sana kuwa wenyeji wa mechi hiyo ya miji miwili kutoka kwa maeneo hayo mawili, ambayo wakaazi wake hawakuweza kuvuka kutoka eneo moja hadi jingine kwa muda wa miaka mitatu, kutokana na makundi tofauti ya Kiislamu kudhibiti maeneo yao.

Eneo la Hiiraan lilikuwa chini ya Al-Shabaab, na eneo hilo lingine lilikuwa chini ya kundi ambalo linapinga utumizi wa silaha la Ahlu sunna Wal Jama'a, na ambalo lina uhusiano mzuri na serikali ya Somalia na pia jamii ya kimataifa.

"Ingawa timu yangu ya nyumbani ya wilaya imeshindwa, ninafurahi sana kwamba tutaweza kuvuka mipaka ya wilaya na kuendeleza mashindano ya soka, na shukrani zangu ni kwa shirkisho la soka nchini Somalia, kwa kusaidia katika kuimarisha soka kati ya mataifa haya", mwenyekiti Abdirashid Aden Roble alieleza.

Image caption Manahodha wa timu zilizocheza mwishoni mwa wiki

Katibu mkuu wa shirikisho la soka la Somalia, Abdi Qani Said Arab alizisifu wilaya zote mbili.

"Hili ndilo jambo ambalo shirikisho la soka la Somalia limekuwa likitazamia, na tunatumaini maendeleo haya ya soka yatachangia katika kuimarisha mashindano ya kabumbu katika maeneo mbalimbali nchini", alielezea katibu mkuu wa SFF kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu.

Alisema shirikisho la SFF mapema mwaka huu lilikuwa limeanzisha mpango wa kuyasaidia maeneo ambayo yalitilia maanani juhudi za kuimarisha soka.

Mafunzo yaliyofanyika katika jimbo la Gal-Mudug mwezi uliopita yalikuwa na nia ya kuimarisha soka katika eneo hilo, na baadhi ya vijana waamuzi waliopata mafunzo tayari wameanza kusimamia mechi.