Rice kuondoka Arsenal

Pat Rice
Image caption Anaondoka Arsenal baada ya kuhudumu kwa zaidi ya miaka 44

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amemsifu msaidizi wake katika klabu, Pat Rice, ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu huu, baada ya miaka 44 akiwa na 'Gunners'.

Mrithi wake atakuwa ni mlinzi wa zamani wa Arsenal, Steve Bould. Rice, ambaye aliichezea Arsenal katika mechi zaidi ya 500, alijiunga na wafanyikazi wa klabu ya Arsenal mwaka 1996, wakati Mfaransa Arsene Wenger alijiunga na klabu kama meneja.

Kama meneja msaidizi, Rice aliisaidia Arsenal kufanikiwa kupata ushindi wa ligi ya Premier mara tatu, na mara nne kulitwaa Kombe la FA.

Meneja Wenger amesema ni vigumu kukadiria kazi aliyoifanya Rice, na kuelezea kwamba ni jambo la "huzuni, huzuni, huzuni sana, na binafsi namshukuru kwa mchango wake katika kunisaidia wakati wangu na ningependa anisamehe kwa baadhi ya shida alizozipata katika kipindi alichokuwa chini yangu, lakini alikuwa ni msaidizi mwaminufu sana, na ninamshukuru kwa kuwa kando yangu kwa muda mrefu hivyo".