Roberto Martinez kuamua

Roberto Martinez Haki miliki ya picha AP
Image caption Martinez kuamua iwapo atasalia Wigan ama ataelekea Liverpool

Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Wigan, Dave Whelan, anakusudia kuweka tarehe maalum na ambayo meneja Roberto Martinez ataizingatia na kuamua iwapo atasalia kama meneja wa klabu hiyo, ama ataondoka.

Martinez aliruhusiwa kuzungumza na klabu ya Liverpool, baada ya pengo la kazi ya meneja kujitokeza katika uwanja wa Anfield.

Raia huyo wa Uhispania pia amehusishwa na klabu ya Aston Villa.

Mwaka jana alikataa kuikubali kazi hiyo ya meneja katika klabu ya Villa.

"Roberto atakuwa Barbados hadi Jumanne ijayo, na atakaporudi, nitatatoa ratiba ya siku saba, na katika muda huo, ninatazamia atakuwa amefanya uamuzi", alisema Whelan.

"Nafahamu kwa hivi sasa kila mtu hajui kinachofanyika, lakini itafika wakati ambapo sote tutahitaji kupata jibu, kwa njia moja au nyingine."

"Hili ni jambo ambalo linajivuta, lakini ninachojali mimi ni kitu kimoja, hatma ya Wigan Athletic. Hakuna chengine ninachojali."

"Ni muhimu tupate suluhu ya suala hili vilivyo, kadri itakavyowezekana, ili tuweze kujiandaa kwa msimu mpya kikamilifu".

Liverpool bado hawajaanza rasmi utaratibu wa kuwahoji watu inaodhaniwa wanaweza kuchukua madaraka hayo ya meneja, baada ya kumfuta kazi Kenny Dalglish, tarehe 16 Mei.

Whelan ana matumaini kwamba Martinez atasalia katika klabu ya Wigan, na katika gazeti la Wigan Evening Post, amenukuliwa akisema: "Lazima nisisitize kwamba sijaamua kukaa tuli na kukubali kumpoteza Roberto kwa timu ya Liverpool."