Terry aadhibiwa na UEFA

Mlinzi wa klabu ya Chelsea, John Terry, atazikosa mechi mbili msimu ujao utakapoanza wa mechi za Ulaya, kufuatia adhabu ya UEFA kumzuia asicheze katika mechi tatu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Aongezewa adhabu kwa kumpiga kwa goti mchezaji wa Barcelona

Tayari aliikosa fainali dhidi ya Bayern Munich, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa nusu fainali, wakati Chelsea ilipopambana na Barcelona.

Lakini UEFA sasa imeamua kumuongezea adhabu, kwa kumkataza kucheza katika mechi mbili zaidi.

Terry pia hatakuwepo katika mechi ya Kombe la Super dhidi ya washindi wa ligi ya Europa, Atletico Madrid ya Uhispania, itakayochezwa mwezi Agosti, na vile vile mechi ya kwanza ya Chelsea katika hatua ya makundi ya kufuzu kwa ligi ya klabu bingwa Ulaya.

Terry na Chelsea wana muda wa siku tatu kuamua ikiwa watakata rufaa au la kufuatia uamuzi huo.

Terry, mwenye umri wa miaka 31, alitolewa kadi nyekundu na mwamuzi, kufuatia kushindilia goti lake dhidi ya mchezaji wa Barca, Alexis Sanchez, pasipo hata mpira kuwa karibu, wakati Chelsea ilikuwa tayari imefungwa bao 1-0 usiku huo.

Aliwaomba msamaha wenzake kwa kuwaletea fedheha.

Hata hivyo licha ya kuondolewa Terry katika mechi hiyo, hatua hiyo haikuinyima Chelsea ushindi, kwani hatimaye iliondoka kwa sare ya 2-2, na katika uwanja wa Nou Camp, waliibuka washindi kwa jumla ya magoli 3-2.

Kisha baada ya hapo walipata ubingwa wao wa kwanza katika fainali ya klabu bingwa, licha ya kuwakosa wachezaji mahiri Terry, Ramires, Branislav Ivanovic na Raul Meireles.