Ureno yaitoa jasho Ujerumani

Ureno Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Timu ya Ureno ilionyesha haikuwa na mchezo wa kusisimua

Bao la Mario Gomez ambalo lilifungwa kwa kichwa na katika dakika za mwishomwisho katika mechi ya pili Jumamosi dhidi ya Ureno liliiwezesha Ujerumani kuondoka na ushindi wa goli 1-0.

Tangu mwanzo ilionekana kwamba Ureno ilikuwa katika hali nzuri ya kuitatiza timu ya Joachim Loew katika mechi hiyo iliyochezewa uwanja wa Lviv.

Ujerumani ilionekana kumiliki mpira kwa muda mrefu, lakini haikupata nafasi za moja kwa moja za kupata mabao.

Hata hivyo katika kipindi cha pili, Gomez alifanikiwa kufunga, baada ya kuupokea mpira kutoka kwa Sami Khedira, na kuianzishia Ujerumani kampeni safi ya Euro 2012 kwa ushindi huo.

Ureno walionekana kuwa hafifu, na waliamka mara tu baada ya Ujerumani kufunga, lakini ikawa vigumu kusawazisha.

Pepe aligonga mwamba, na baadaye hayo pia yakampata Nani, na ilielekea kweli ushindi ulikuwa ni wa Ujerumani.