Czech yajiongezea matumaini

Ugiriki na Czech Haki miliki ya picha AP
Image caption Mabingwa wa mwaka 2004 Ugiriki walilemewa

Juhudi za Jamhuri ya Czech kufanya vyema katika mashindano ya Euro 2012 zilipata nguvu Jumanne, kwa kuishinda Ugiriki magoli 2-1, mabao ya haraka katika dakika sita za mwanzo.

Ugiriki walikuwa mabingwa mwaka 2004, lakini uhodari wao bado haujajitokeza katika mashindano ya mwaka huu.

Petr Jiracek alifunga bao la kwanza katika mechi hiyo, dakika ya tatu.

Vaclav Pilar aliongezea bao la pili.

Ugiriki wakidhani wamepata bao, mwamuzi alilifutilia mbali kwa kusema walikuwa wameotea.

Hata hivyo, katika kipindi cha pili, kufuatia kosa la kipa wa Czech, Peter Cech, Ugiriki waliweza kujituliza kwa goli moja kupitia Fanis Gekas.

Cech, mwenye umri wa miaka 30, na ambaye ni kipa makini katika klabu ya Chelsea, katika mashindano haya amefungwa magoli matano tayari, lakini bila shaka atashukuru aliweza kuepuka makosa zaidi, na nchi yake ikaondoka na ushindi.