England yapata ushindi wa kusisimua

England na Sweden
Image caption England imeiondoa Sweden katika mashindano ya Euro 2012

Danny Welbeck aliweza kuandikisha bao la ushindi la England dhidi ya Sweden, katika mechi ya kusisimua ya kundi D.

England iliweza kutangulia kwa bao la kwanza wakati Andy Caroll alipofunga kwa kichwa, baada ya kuletewa mpira wa juujuu kutoka kwa Steven Gerrard.

Lakini mlinzi Olof Mellberg aliweza kufunga bao la kusawazisha, na baadaye kupata la pili kwa kichwa na kuiwezesha Sweden kuongoza kwa mabao 2-1.

Mchezaji wa zamu Theo Walcott kupitia mkwaju kutoka yadi 25 aliiwezesha England kusawazisha, na kisha baadaye alipompigia mpira Welbeck, akafanikiwa kufunga bao la tatu na la ushindi, na kuhakikisha Sweden wanaelekea nyumbani baada ya kuwaondoa katika mashindano ya mwaka huu ya Euro 2012.

Huu ndio ushindi mkubwa zaidi wa England dhidi ya timu ya Sweden, na mara tu baada ya Carroll kuwawezesha kuongoza, England haikuona tena kitisho kikubwa mno cha kulemewa katika mechi hiyo ya Ijumaa.

Pengine onyo la nahodha Steven Gerrard kabla ya mechi katika kuhakikisha mshambulizi Zlatan Ibrahimovic asipate nafasi za kufunga labda ziliweza kuisaidia England kuepuka kushindwa.

Lakini kwa kumzuia Ibrahimovic, pengine ndio maana mchezaji mwenzake Melberg alipata bao la pili la Sweden kwa urahisi kwa kuwa England hawakumzuia kikamilifu.

Meneja wa England Roy Hodgson kisha aliamua kumtumia Walcott, na bila shaka mchezaji huyo alibadilisha mchezo.