Ukraine yashindwa kuwika nyumbani

Ukraine na Ufaransa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mechi ilichezwa katika uwanja ulioloa maji

Ufaransa ilipata ushindi wake wa kwanza katika kundi D katika mechi ya Ijumaa ya Euro 2012, baada ya kuwashinda wenyeji Ukraine katika uwanja ulioloa maji kufuatia mvua kubwa katika uwanja wa Donetsk.

Mchezo ulisitishwa baada ya dakika nne tu, kufuatia uwanja kuloa, na timu zilirudi uwanjani baada ya saa nzima kupita.

Lakini waliporudi, kulikuwa hakuna njia nyingine ya kuiokoa Ukraine, kuanzia wakati Jeremy Menez, mchezaji wa St Germain ya Ufaransa, alipowaongoza Wafaransa katika kufunga mabao, akitumbukiza mpira kutoka yadi 12.

Yohan Cabaye alifunga bao la pili.

Hilo lilikuwa ni bao la kwanza katika mechi ya kimataifa kwa mchezaji huyo wa klabu ya Newcastle inayocheza katika ligi kuu ya England.

Bao hilo lilipatikana kwa urahisi kufuatia kosa la wachezaji wa ulinzi wa Ukraine namna walivyocheza katika uwanja huo wa Donbass Arena.

Wachezaji wa timu zote walikuwa na kibarua kigumu katika kucheza katika hali ya joto kali na uwanja ulioloa, na ndio maana mwamuzi Bjorn Kuipers kutoka Uholanzi awali alikuwa ameamua kusitisha mechi hiyo.

Ilibidi juhudi za dharura kufanyika ili kuyafyonza maji hayo, na baadaye mwamuzi kuidhinisha mechi kuendelea.