Wenyeji Poland nje!

Jamhuri ya Czech
Image caption Ushindi wa Czech umewaondoa wenyeji Poland

Petr Jiracek alifunga bao la pekee katika mechi ya uwanja wa Wroclaw dhidi ya wenyeji Poland siku ya Jumamosi, na kuwahuzunisha mashabiki wa nyumbani, wakati Jamhuri ya Czech ilipofuzu kuingia robo fainali za mashindano ya Euro 2012.

Jamhuri ya Czech imefuzu katika kundi hilo, baada ya kuongoza kwa pointi 6.

Jiracek, kiungo cha kati wa timu ya Wolfsburg ya Ujerumani, aliweza kuutambariza mpira wavuni katika sehemu ambayo kipa Przemyslaw Tyton hakuweza kuwa na matumaini kabisa ya kuufikia mpira, zikiwa zimesalia dakika 18 tu mechi hiyo kumalizika.

Poland walianza mechi wakifahamu kwamba iwapo wangelipata ushindi katika mechi hiyo, basi wangeliweza, kwa mara ya kuwanza, kuwa miongoni mwa timu nane ambazo zingelisalia katika mashindano kushiriki katika mechi za robo fainali.

Nahodha wa Poland Jakub Blaszczykowski, katika juhudi za dakika ya mwisho alikuwa nusra afunga bao la kusawazisha, lakini ulinzi wa Czech ulikuwa thabiti, na mpira kuondolewa kabla ya kuvuka msitari.