Hasira za Nalbandian

McDougall na Nalbandian
Image caption Msaidizi wa mwamuzi aliyejeruhiwa na Nalbandian

David Nalbandian aliondolewa katika fainali ya mashindano ya tennis ya Aegon katika uwanja wa Queen mjini London, kwa kulipiga teke bango la matangazo na ambalo lilimuumiza msaidizi wa mwamuzi.

Mchezaji huyo kutoka Argentina, na ambaye anashilia nafasi ya 39 katika orodha ya wachezaji bora wa tennis duniani kwa upande wa wanaume, aliomba radhi baadaye kwa kitendo hicho cha utovu wa nidhamu.

Nalbandian, mwenye umri wa miaka 30, alikuwa akipambana na Marin Cilic kutoka Croatia.

Nalbandian, kabla ya kuzidiwa na hasira, alikuwa akiongoza kwa 7-6 (7-3) 3-4 alipoupiga teke ubao uliokuwa mbele ya kiti cha Andrew McDougall, na kumuumiza mguu kiasi cha damu kumtoka.

Mwamuzi mkuu, Fergus Murphy, baada ya kitendo hicho alimpa ushindi Cilic, na afisa wa mashindano ya tennis ya ATP, Tom Barnes, akaidhinisha uamuzi huo.

"Ninasikitika sana kwa hayo, wakati mwingine unakerwa na mambo ukiwa uwanjani," alisema Nalbandian.

Wakati maafisa walipokuwa wakishauriana wachukue hatua gani, baadhi ya mashabiki 6,000 waliokuwa uwanjani walitaka pambano hilo kuendelea.

"Wakati mwingine hufanya kosa, na ikiwa ni hivyo, ninakubali nimekosa," alisema Nalbandian.

"Ni hali mbaya kukamilisha mechi kwa njia hii, lakini wakati mwingine tunahisi tumelewa mno kutokana na mechi nyingi za ATP tunazocheza katika mashindano mbalimbali."

"Leo nimefanya kosa. Wakati mwingine inabidi nikubali nimefanya kosa, na kila mtu hufanya makosa. Lakini ninahisi mchezo huu haikufaa kumalizika katika hali hii - hasa kwa kuwa ni fainali."