Ureno imo katika robo fainali

Ureno Haki miliki ya picha AFP
Image caption Cristiano Ronaldo aliiwezesha Ureno kuingia robo fainali

Mabao mawili ya mshambulizi Cristiano Ronaldo yaliiwezesha Ureno kuingia robo fainali ya michuano ya Euro 2012, kwa kuifunga Uholanzi, na pasipo shaka yoyote, kuwalazimisha kurudi nyumbani.

Kwa Uholanzi kuwa na matumaini yoyote kuendelea kusalia katika mashindano hayo, walilazimika kuifunga Ureno magoli 2-0, na bao la kwanza la mkwaju wa kupinda kutoka kwa Rafael van der Vaart liliwapa matumaini Uholanzi walipoweza kutangulia.

Lakini mchezo wa Uholanzi uliendelea kufifia, na Ronaldo alifanikiwa kusawazisha, alipopigiwa mpira na mwenzake Joao Pereira.

Nani alimsaidia Ronaldo kufunga kwa mara ya pili, na Ureno ikavuka hatua ya makundi na kujiandikishia nafasi katika robo fainali.

Ureno sasa itacheza na Jamhuri ya Czech, inayoongoza kundi A.

Kwa Uholanzi, timu hiyo imeonyesha mchezo duni sana, kwa kushindwa katika mechi tatu za makundi, ilhali miaka miwili iliyopita, wao walimaliza katika nafasi ya pili katika fainali ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Itawachukua muda Uholanzi kumsahau Ronaldo, mchezaji nyota wa Real Madrid ya Uhispania, ambaye aliifungia klabu hiyo magoli 60 msimu uliopita, na katika mechi dhidi ya Jumapili alicheza kwa kasi na kwa juhudi na kuwaacha Waholanzi wamezubaa.