Murray kuandikisha historia

Andy Murray
Image caption Anaweza kuwa Muingereza wa kwanza kufika fainali ya Wimbledon baada ya miaka 74

Andy Murray atakuwa Muingereza wa kwanza kupambana katika fainali ya Wimbledon katika kipindi cha miaka 74, ikiwa atafuzu kwa hatua hiyo, kama atamshinda Mfaransa Jo-Wilfried Tsonga katika nusu fainali ya Ijumaa.

Murray, kwa mara ya nne mfululizo, atakuwa anapambana katika nusu fainali, baada ya kumshinda David Ferrer kutoka Uhispania.

Mchezaji wa mwisho, raia wa Uingereza aliyefuzu kwa fainali ya Wimbledon alikuwa ni Bunny Austin, mwaka 1938, miaka miwili baada ya ushindi wa Fred Perry.

Bingwa mtetezi Novak Djokovic kutoka Serbia atapambana na mshindi mara sita, Roger Federer kutoka Uswisi, katika pambano la kwanza la nusu fainali, saa tisa za Afrika Mashariki.

Murray, mwenye umri wa miaka 25, na aliyepangwa katika nafasi ya nne miongoni mwa wachezaji bora zaidi wa kiume katika mashindano ya Wimbledon, amemshinda Tsonga mara tano katika mapambano sita ambayo wamewahi kukutana.

Lakini Murray, ambaye katika nusu fainali mbili zilizopita alishindwa na Rafael Nadal kutoka Uhispania katika mashindano hayo, amesisitiza kamwe hana dharau kwa mchezaji Tsonga, na aliyepangwa katika nafasi ya tano, na ambaye licha ya kulemewa, aliweza kujikakamua na kumshinda Federer miezi 12 iliyopita.