Federer amnyima Murray ushindi

Federer na Murray Haki miliki ya picha Getty
Image caption Murray aliwavunja moyo Waingereza waliotazamia ushindi wa Wimbledon baada ya miaka 76

Roger Federer kutoka Uswisi leo Jumapili aliibuka bingwa wa mashindano ya Wimbledon kwa mara ya saba, baada ya kumshinda Andy Murray wa Uingereza 4-6, 7-5, 6-3, 6-4, na kuyavunja matumaini ya Waingereza kuchukua ubingwa wa Wimbledon, licha ya kusubiri kwa miaka 76, tangu Fred Perry alipoibuka mshindi mwaka 1936.

Hii ilikuwa fainali ya kwanza ya Wimbledon kuchezwa huku paa likiwa limeufunika uwanja huo kutokana na mvua. Paa hilo kwa mara ya kwanza lilianza kutumiwa mwaka 2009.

Andy Murray alianza vyema katika pambano hilo la fainali ya Wimbledon dhidi ya Roger Federer. Alifanikiwa kushinda katika seti ya mwanzo, kwa kutangulia kwa 6-4.

Lakini Federer alilipiza kisasi na kuongoza 7-5 katika seti ya pili, huku mvua ikisitisha pambano hilo la fainali.

Ilikuwa inasikitisha kwa mashabiki kumtizama Murray, mwenye umri wa miaka 25, akitokwa na machozi baada ya kukosa kuibuka mshindi, kufuatia kushindwa kwa mara ya nne katika fainali ya mashindano makubwa ya Grand Slam.

Federer aliweza kuifikia rekodi iliyoandikishwa na Mmarekani Pete Sampras, na kwa ushindi huo, ataongoza katika orodha ya wachezaji bora zaidi wa kiume duniani.

Murray alikuwa Muingereza wa kwanza kucheza katika fainali ya Wimbledon ya mchezaji mmoja kwa mmoja, tangu Bunny Austin alipofikia hatua hiyo mwaka 1938.