Webber mshindi wa Silverstone

Mark Webber Haki miliki ya picha AFP
Image caption Webber pamoja na Alonso wa timu ya Ferrari ndio madereva waliofanikiwa kuibuka washindi katika mashindano mawili msimu huu

Mark Webber, dereva wa timu ya Red Bull, siku ya Jumapili aliibuka bingwa wa mashindano ya Uingereza ya magari ya Grand Prix.

Dereva huyo kutoka Australia, aliweza kumpita Fernando Alonso kutoka Uhispania, katika raundi za mwishomwisho za mashindano hayo ya Silverstone.

Alonso aliweza kuongoza kwa muda mrefu tangu mwanzo wa mashindano, lakini Webber aliweza kutumia mbinu kwa upande wa kubadilisha magurudumu, na hatimaye kuweza kufukuzana kwa kasi na dereva huyo wa Uhispania.

Alonso hatimaye alimaliza katika nafasi ya pili, na Mjerumani Sebastian Vettel, dereva wa timu ya Red Bull, alimaliza katika nafasi ya tatu.

Felipe Massa, kutoka Brazil, na akiwa ni dereva wa Ferrari, alimaliza katika nafasi ya nne.

Lewis Hamilton, dereva wa McLaren, ilibidi aridhika na kumaliza katika nafasi ya nane, huku Muingereza mwenzake, Jenson Button, na pia akiwa katika timu ya McLaren, akishikilia nafasi ya 10.

“Nimewahi kuibuka mshindi mara chache, lakini ushindi huu bado haujaniingia akilini. Nilipata nafasi moja ya kuongoza, na kamwe sikutazamie iniepuke,” alielezea Webber.

Webber sasa yumo katika nafasi ya nne katika kuwania nafasi ya dereva bora zaidi msimu huu, akiachwa na Alonso kwa pointi 37 sasa.

Vettel yumo katika nafasi ya tatu, na tofauti kati yake na Alonso ni pointi 29.

Timu ya McLaren, ambayo ilianza msimu ikiwa na gari lenye kasi zaidi, sasa inaelekea wanaendelea kuachwa nyuma na Red Bull na Ferrari, ambayo wamweza kuimarisha magari yao zaidi.

Mashindano ya Silverstone yaliamuliwa kupitia magurudumu.

Huku Ferrari wakiamua kumuanzisha Alonso kwa kutumia magurudumu magumu zaidi, kama walivyofanya mafundi wa McLaren pia waliohusika na Hamilton, kinyume na hayo, Red Bull waliamua kutumia matairi ya kawaida yaliyo mepesi zaidi.

Ushindi huu umemfanya Webber, kama Alonso, kuwa madereva wawili wa pekee msimu huu ambao wameweza kuibuka washindi katika mashindano mawili.