Maradona atemwa na klabu ya Dubai

Maradona na Al Wasl Haki miliki ya picha elvis
Image caption Maradona na Al Wasl

Mcheza soka mashuhuri duniani na nyota ya Argentina, Diego Maradona amefutwa kazi kama Meneja wa klabu ya nchini Imarati Al Wasl baada ya kuiongoza kwa kipindi cha miezi 14.

Mkongwe huyo alianza kuingia mashaka mnamo mwezi Juni baada ya bodi nzima ya uongozi wa klabu kujiuzulu kufuatia matokeo yasiyoridhisha na kuhitimisha msimu mzima bila kombe lolote.

Maradona, mwenye umri wa miaka 51 alijiunga na klabu hio yenye makao yake mjini Dubai mwezi May mwaka 2011 na hadi kupigwa mkasi alikuwa na mwaka mmoja uliosalia kwenye mkataba wake.

Msimu uliopita klabu yake ya Al Wasl ilimaliza katika nafasi ya nane.

Taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha Bodi ya wakurugenzi wa Al Wasl football company kutathmini uongozi wa Diego Maradona na wasaidizi wake, uwamuzi umefikiwa wa kumfuta kazi Maradona pamoja na wasaidizi wake.

Itakumbukwa kuwa Maradona mshindi wa Kombe la Dunia akiichezea nchi yake Argentina mnamo mwaka 1986 alitia for a mwaka huu alipokabiliana na mashabiki wa upinzani kwa ujasiri.

Wakati wa mechi ambayo klabu yake Al Wasl ilichapwa 2-0 na Al Shabab,inafahamika kuwa alikimbia hadi kiti alichokuwa amekaa mke wake ili mashabiki waliokua wamejaa hasira wasimdhuru baada ya kuwarushia matusi wake na marafiki wa wachezaji wake.

Maradona aliajiriwa ili kuizidishia umaarufu klabu ya Al Wasl ndani na nje ya uwanja, lakini ilimaliza msimu ikiwa nyuma ya mshindi wa Ligi Al Ain kwa pointi 29.