Alonso ashinda Grand Prix ya Ujerumani

Fernando Alonso ameshinda mashindano ya mbio za magari ya Grand Prix ya Ujerumaini kwa Ferrari yake siku ya Jumapili akiendelea kuongoza katika mbio hizo za Formula One.

Bingwa mtetezi wa mara mbili mfululizo wa mashindano hayo Sebastian Vettel wa timu ya Red Bull, kwa mara nyingine ameshindwa kupata ushindi nyumbani kwake, lakini alimpita Jenson Button wa McLaren ukisalia mzunguko mmoja katika mizunguko 67 kwa nafasi ya pili.

Button alisumbuliwa na matatizo ya matairi katika mizunguko michache ya mwisho baada ya kumpatia changamoto Alonso katika kuongoza.

Alonso alikuwa dereva wa kwanza kushinda mbio tatu katika msimu huu.

Baada ya kusheherekia kwa kufungua champagne na kuhojiwa jukwaani na bingwa wa mara tatu Niki Lauda Alonso alisema: ''Ilikuwa ngumu, si mashindano rahisi.

"Labda tulikuwa wepesi, lakini tulikuwa washindani thabiti kuweza kuongoza pamoja na mpangilio mzuri kutoka katika timu. "Baada ya kituo cha pili, nilipokabiliwa na ugumu, gari lilikuwa katika hali nzuri na katika kasi ya juu kabisa kutawala mashindano.''

Hata hivyo Vettel, alikuwa akimlalamikia Hamilton alipojiweka pembeni ya mzunguko akisema: ''Sikuona umuhimu wowote wa kufanya hivyo.

"Ilikuwa ni upuuzi kiasi fulani kukanganya waliotangulia. Kama alitaka kuongeza kasi, angerudi nyuma na kutafuta upenyo na kuongeza kasi tena. Kwa ujumla sifurahii kabisa''

Akimzungumzia uchunguzi wa Vettel kuhusu hatua yake kuwapita ghafla wenzake, Button alisema: ''Hakuna cha kuzungumza. Kamera za Televisheni zinaelezea kila kitu. ''Ni bora niongelee mashindano. Yalikuwa mazuri, niliyafurahia sana.''