Yanga na APR zafuzu

Yanga ya Tanzania Haki miliki ya picha Yanga
Image caption Mabingwa watetezi Yanga wamefuzu kuingia nusu fainali ya Kombe la Kagame

Klabu bingwa mtetezi Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya Tanzania, imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Kagame baada ya kuitoa timu ya Mafunzo ya Zanzibar kwa mikwaju ya penalti.

Matokeo hadi mwisho wa mchezo mjini Dar es Salaam siku ya Jumatatu yalikuwa 1-1, Mafunzo wakiwa wa kwanza kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Ali Mmanga.

Yanga walifanikiwa kusawazisha dakika ya kwanza kipindi cha pili kupitia kwa Said Bahanuzi na kufanya mchezo uamuliwe kwa penalti baada ya dakika tisini, na Yanga kushinda kwa penalti tano kwa nne.

Yanga watacheza na APR ya Rwanda, ambao nao wametinga nusu fainali baada ya kuwatoa URA wa Uganda kwa mabao 2-1.

APR walipata mabao yao kipindi cha kwanza kupitia kwa Jean Claude Iranzi na Seleman Ndikumana, wakati bao la URA lilifungwa na Robert Ssentongo kipindi cha pili.

Kocha wa APR Mholanzi Ernest Bradnt anasema itakuwa mechi ya kulipiza kisasi; “Yanga walitufunga hatua ya makundi, hivyo tutahitaji kulipiza kisasi. Lakini pia tumeshinda kombe hili mara tatu nyumbani na sasa tunataka kulishinda ugenini, hapa Tanzania,” alisema.

Jumanne Simba itacheza na timu mpya kwenye mashindano haya, Azam, pia kutoka Tanzania, na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itacheza na Atletico ya Burundi.