Azam na Vita waingia nusu fainali

Kocha Stewart Hall
Image caption Kocha Stewart Hall akiwa na wachezaji wa timu yake ya Azam

Vilabu vya Azam na Vita vimefanikiwa kuingia nusu fainali ya michuano ya soka ya Cecafa.

John Bocco alikuwa shujaa pale timu yake ya Azam ya Tanzania, ilipofanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuwafunga mabingwa wa Tanzania, Simba, mabao 3-1.

Katika mechi hiyo ya robo fainali iliyochezwa Jumanne mjini Dar es Salaam, Bocco alifunga mabao yote dakika ya 17, 46 na 73, wakati bao la kufutia machozi la Simba lilifungwa na Shomari Kapombe dakika ya 53.

Timu hiyo sasa itapambana na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwenye nusu fainali itakayochezwa Alhamisi.

Vita Club walifuzu baada ya kushinda kwa mambao 2-1 dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye mechi nyingine iliyochezwa Jumanne. Mabao ya Vita yalifungwa na Taddy Etekiama na Basilua Makola wakati bao la Atletico lilifungwa na Pierre Kwizera.

Matokeo hayo yamekuwa ya kushangaza hasa ikizingatiwa kuwa Simba ni timu kongwe ambayo imeshinda kombe hili la ukanda mara sita.

Nayo Azam, iliyoanzishwa mwaka 2007, haya ni mashindano yao ya kwanza kimataifa tangu timu ianzishwe na ilipata tiketi ya kushiriki baada ya kumaliza ligi msimu uliopita ikiwa nafasi ya pili.

Mafanikio ya Azam yanakuja baada ya kusajili wachezaji kutoka Ivory Coast na Kenya na kumwajiri kocha kutoka Uingereza.

Mechi zote za nusu fainali zitachezwa Alhamisi kufuatia kuondoshwa Simba kwenye mashindano.

Timu nyingine zitakazokutana kwenye hatua hiyo ni bingwa mtetezi Yanga ya Tanzania na APR ya Rwanda.

Fainali itachezwa Jumamosi na bingwa atapewa zawadi ya dola 30,000 na mshindi wa pili 20,000, na atakayemaliza katika nafasi ya tatu ataondoka na kitita cha dola 10,000.