Bolt asema amejiandaa kikamilifu

Usain Bolt
Image caption Bolt anasema anataka kuandikisha historia mjini London

Usain Bolt amesema amejiandaa kikamilifu kuutetea ubingwa wake wa mashindano ya Olimpiki katika mbio fupi, licha ya kwamba kwa hivi sasa anasema yeye ni mzima asilimia 95.

Bolt, bingwa wa mbio za mita 100 na 200, anasema kwa kiasi fulani ameweza kupata nafuu baada ya kupambana na matatizo ya mgongo na misuli, na anahisi ataweza kuutetea ubingwa wake katika mbio hizo fupi.

Mwanariadha huyo wa Jamaica, akizungumza na mwandishi wa michezo wa BBC, David Bond, amesema licha ya kwamba yeye si mzima kwa asilimia 100, ataweza kuhifadhi ubingwa huo, na kuandikisha historia mjini London.

Bolt alitamka hayo ikiwa sasa ni miaka minne tangu alipovunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 100 katika mashindano ya Beijing ya mwaka 2008, kwa kuandikisha muda wa sekunde 9.69, licha ya kupunguza kasi na kuanza kufanya sherehe hata kabla ya kuvuka msitari wa kukamilisha mbio.