Maelezo juu ya shughuli za ufunguzi

Imeandikwa na Israel Saria

Sherehe zilizosimulia kiwango cha juu cha ubunifu kupitia historia ya mchangamano wa Taifa la Uingereza ambalo ni mwenyeji, zilidumu zaidi ya saa tatu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Malikia akiwasili kwa sherehe

Vifijo na nderemo vilitawala uwanja mkuu wa michezo hiyo jijini London, na mapigo ya fataki hayakuwa ya kawaida, kuashiria marejeo ya michuano hiyo jijini hapo baada ya miaka 64.

Wapo waliojua ni utani au mzaha, lakini wengine walishituka, wakidhani Malkia Elizabeth II aliruka kwa parachuti na Daniel Craig (James Bond) kutoka kwenye ndege.

Hiyo ilikuwa baada ya Malkia Elizabeth II kuoneshwa akiwa kwenye kasri yake ya Buckingham, akijiandaa kutoka ili kupanda ndege na kwenda kujiunga na watu karibu 80,000 waliokuwa uwanjani.

Miongoni mwa halaiki iliyokuwa uwanjani ni wanamichezo wa Afrika Mashariki, kwa namna ya pekee Kenya, Tanzania na Uganda.

Kenya inajivunia rekodi yake, hasa kwenye riadha, ambapo mwanariadha anayeshika rekodi ya dunia, David Rudisha anapewa nafasi kubwa kwenye mbio za mita 800.

Kenya ina jumla ya wanamichezo 47, akiwamo mshindi wa mbio za marathon jijini London mwaka jana, Mary Keitany. Kana kwamba hiyo haitoshi, Kenya inaingia kwa kujiamini zaidi, kwani wana mruka vihunzi mahiri, Brimin Kipruto anayenyemelea medali ya tatu mfululizo katika Olimpiki.

Uganda ina wanamichezo 16 kwenye mashindano haya ya Olimpiki. Nahodha wa timu hiyo, Ganzi Mugalu alibeba bendera ya taifa kwa uchangamfu mkubwa.

Image caption Moses Kipsiro

Wanaopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri ni pamoja na waliotwaa medali mbli za dhahabu kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka juzi, Moses Ndiema Kipsiro katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000.

Ijumaa usiku katika maandamano, Uganda waliingia uwanjani wakiwa wa 192 kati ya nchi 205 zinazoshiriki mashindano hayo.

Bila shaka subira yao kuingia uwanjani italipa katika hadhi ya medali watakazotwaa.

Kwa upande wa Tanzania, ina wanamichezo wachache ikilinganishwa na wa baadhi ya nchi, ambazo wanamichezo wake walikuwa kana kwamba wamesongamana.

Tanzania inawakilishwa na wanamichezo saba, chini ya kiongozi wa msafara, Hassan Jarufu. Mkuu huyo wa msafara alionesha imani ya kufanya vyema, baada ya vijana wake kufanya mazoezi katika Chuo Kikuu cha Bradford kwa wiki mbili.

Image caption Bendera ya Tanzania

Msafara mzima unajumuisha wachezaji saba, makocha watatu, madaktari wawili na mkuu wa msafara, na kazi ni kama tayari imeanza London hivi sasa. "Kila kitu kinakwenda vizuri," ndiyo kauli ya Jarufu, japokuwa imekuwa ndoto za alinacha kuvunja rekodi iliyowekwa na akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kwa kupata medali za fedha.

Pamoja na wingi wa nchi zilizoshiriki, zikiingia kwa kufuata alfabeti isipokuwa wenyeji Uingereza na waasisi Ugiriki, wadau wa kila nchi walisubiri hadi kukata kiu yao. Ilikuwa fursa ya sekunde chache kwa kila nchi kuonekana kwenye televisheni, lakini muhimu wake ni mkubwa, ambapo wazalendo walifurahi kuona msafara wa wawakilishi wake ukipeperusha bendera za nchi zao.

Sherehe zilikwenda vyema, zikiwa zimetanguliwa siku moja kabla na michezo mbalimbali kwenye viwanja tofauti na pale, ikiwa ni pamoja na soka ya wanaume na wanawake.

Wachambuzi wanaona kwamba sherehe za mwaka huu zimefunika zile za Beijing, China kwenye Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008. Matukio tofauti yaliyobuniwa na kuchanganywa chini ya uratibu wa mkurugenzi na mtayarishaji filamu, Danny Boyle, yalijikita katika historia tajiri ya Uingereza.

Walianza na maisha ya vijijini zamani kabisa, wasanii wakiigiza hata aina ya mavazi na sura za watu wake.

Waliendelea kwa kuieleza hadhira enzi za mapinduzi ya viwanda, wakati huo Uingereza ikiwa ndiyo kama karakana ya dunia na kiongozi kwenye utajiri wa viwanda mbalimbali.

London na Uingereza ya sasa, ambayo vijana ndiyo wanaijua, na pengine kuielewa zaidi, haikusahauliwa, kwani wasanii hao walionesha jinsi sayansi na teknolojia ilivyoifikisha nchi mbali.

Kubwa lililodhihirishwa pia, ni utajiri wa utamaduni mchanganyiko nchini Uingereza, likiwa ni taifa linalojumuisha watu wa asili na rangi mbalimbali, lakini wanakaa pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano. Hiyo ndiyo dhima kubwa ya michezo pia.

Ni kwa msingi huo, waliojua thamani ya maandalizi yake waliridhishwa na matumizi ya Pauni milioni 27. Wakati maelfu ya watu walifika uwanjani kushuhudia viongozi wa nchi na serikali zaidi ya 100 wakienzi michezo hii mikubwa zaidi duniani, wengine kwa mamilioni walishuhudia moja kwa moja kwenye televisheni, wakiwa katika mabara tofauti duniani.

Waziri Mkuu, David Cameron ambaye amekuwa na msimamo thabiti juu ya umuhimu wa kuandaa mashindano kama haya, alionekana akifuatilia kwa makini, huku Malkia Elizabeth II na Prince Philip wakionekana thabiti tangu mwanzo hadi walipoondoka.

Maelfu ya watu walisafiri hadi London kwa ajili ya ufunguzi huo, na wengine kwa ajili ya kuendelea na mashindano hadi timu wanazoshangilia zitakapofungishwa virago.

Kwa ujumla wake, pamoja na kufika kutazama michezo hiyo, wapo maelfu wengine wanaochukua fursa hiyo kufanya utalii nchini Uingereza, jambo ambalo Cameron alisema ni muhimu, alipowataka wanamichezo wa Uingereza wafanye vizuri ili wazidi kuitangaza nchi.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Malkia kwenye sherehe ya ufunguzi

Pengine wasomi na watafiti watavutwa zaidi na saa tatu unusu za sherehe zile, kwa sababu zilisheheni falsafa ya hali ya juu, baadhi ya mambo yakiwa yamejificha nyuma ya pazia, pasipo kuonekana moja kwa moja.

Pamoja na hayo, ilikuwa burudani machoni, na wakati mwingine wasanii waliwafanya watazamaji kulipuka kwa vigelegele kutokana na umahiri wao. Hazikukosekana nyakati zile ambapo baadhi ya watazamaji walijikuta wameduwaa, wakitazama na kufikiria kile kinachotendwa, wakijaribu kuvuta hisia siku hizo zilizopita, ama walizosimuliwa au kusoma vitabuni na kwenye majarida.

Yote kwa yote, ulikuwa ufunguzi mzuri, ambao kama kawaida ulipambwa na muziki mwororo na kuhudhuriwa na watu maarufu katika sekta zote muhimu.

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmedinejad alikuwa kiongozi aliyetarajiwa kuleta utata London na kuumiza viongozi vichwa. Hata hivyo, aliamua kutofunga safari ya Uingereza, akisema sababu ni kwamba Uingereza ina tatizo naye.

Mnururisho wa anga kwa fataki usiku ule, ni ishara ya kazi kubwa ya washiriki, lakini kikubwa kikiwa ni kudumisha urafiki miongoni mwao na nchi zao. Malkia Elizabeth II, alizindua rasmi michuano hiyo baada ya kukaribishwa na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Jacques Rogge. Mwisho.