Senegal,Misri zatolewa soka Olympic

Timu ya Senegal na Misri zimetolewa katika mechi ya mchezo wa robo fainali mashindano ya soka kwa wanaume katika michezo ya London Olympics 2012.

Senegal imefungwa magoli manne kwa mawili na Mexico katika mashindano hayo.

Hadi vipindi vyote viwili vinamalizika Senegal na Mexico zote zilikuwa zimefungana mabao mawili kwa mawili, lakini Senegal ilizidiwa nguvu baada ya Mexico kuchomeka magoli mawili zaidi katika kipindi cha ziada.

Nayo timu ya wanaume kutoka Misri ilijikuta ikichapwa mabao matatu kwa sifuri na Japan.

Misri walionekana kuzidiwa na Japan baada ya goli la kwanza kutoka kwa Kensuke Nagai, wakati walipojikuta wakibakia kumi kabla ya mapumziko baada ya mchezaji wao Saad Samir kutolewa nje.

Japan ilifanya mashambulizi kutoka kwa washambuliaji wake Maya Yoshida na Yuki Otsu.

Kufuatia matokeo hayo, sasa Japan na Mexico zimeingia nusu fainali itakayochezwa siku ya Jumanne.