Andy Murray amuangusha Federer

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Andy Murray

Andy Murray wa Timu ya Uingereza hatimaye amefanikiwa kushinda shindano kubwa katika maisha yake ya mchezo wa Tennis kwa kumuangusha mwamba wa mchezo huo Roger Federer katika fainali ya wanaume iliyochezwa uwanja wa Wimbledon.

Murray alimshinda mwakalishi wa Uswizi 6-2 6-1 6-4. Mwakilishi wa timu ya Uingereza hajawahi kumshinda Federer katika mchuano wa seti tano na ni hivi karibuni alishindwa na mchezaji huyo huyo kwenye fainali ya mashindano ya kila mwaka ya Wimbledon.

Pamoja na kumuangusha mchezaji bora duniani Murray amejitokeza kua Muingereza wa kwanza kunyakua medali ya dhahabu ya mashindano ya Olimpiki tangu Josiah Ritchie mnamo mwaka 1908.

Ushindi huu ni nyongeza ya furaha na harusi ya Waingereza wanaoshikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa medali, nyuma ya Uchina na Marekani.

Muingereza wa mwisho kushinda medali ya rangi ya aina yoyote alikua Charles Dixon, aliyeshinda medali ya fedha kwenye mashindano ya mwaka 1920 mjini Antwerp.

Kwenye mchuano wa kuwania nafasi ya tatu na medali ya shaba Juan Martin del Potro wa Argentina amemuangusha mwamba mwingine mchezaji wa pili kwa ubora Novak Djokovic.

Mchezaji huyo akiwa na namba nane kwa ubora katika mchezo wa Tennis amemshinda M-Serbia 7-5 6-4 katika mda wa saa moja na dakika 48 uwanja wa Wimbledon.