Rudisha aandikisha rekodi mpya

David Lekuta Rudisha Haki miliki ya picha PA
Image caption Rudisha akifurahia kuivunja rekodi yake mwenyewe ya awali ya dunia katika mbio za mita 800

David Rudisha, mwanariadha kutoka Kenya, alikuwa wa kwanza kuandikisha rekodi mpya katika mashindano ya Olimpiki ya London mwaka 2012, alipotwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 800.

Rudisha, mwenye umri wa miaka 23, alikamilisha mbio hizo Alhamisi jioni kwa muda wa dakika moja, sekunde 40.91, akikamilisha mbio chini ya muda wa dakika moja na sekunde 41.

Kijana kutoka Botswana, Nijel Amos, alimaliza katika nafasi ya pili na kupata medali ya fedha, huku Mkenya Timothy Kitum ikibidi aridhike na ya shaba kwa kumaliza katika nafasi ya tatu.

Katika mbio hizo, Rudisha, ambaye hata kabla ya mbio za Alhamisi alikuwa ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 800, alitangulia tangu mwanzo, na akikamilisha mzunguko wa kwanza kwa sekunde 49.28, na kumalizia kwa kuongeza kasi, na kuivunja rekodi yake mwenyewe ya awali ya dunia.

Wanariadha wengi katika mbio hizo za mita 800, binafsi waliandikisha muda wao bora zaidi, lakini Abubaker Kaki Khamis kutoka Sudan peke yake ndiye aliyeshindwa kufanya hivyo, na akimaliza katika nafasi ya saba.

Rudisha aliielezea BBC: "Wau! Nimefurahi sana. Hii ni nafasi ambayo nimeisubiri kwa muda mrefu sana. Kufika hapa na kuvunja ni rekodi ni jambo ambalo kamwe sikuamini litatokea."

"Nilikuwa nimejiandaa vyema na sikuwa na shaka nitapata ushindi. Leo hali ya hewa ilikuwa nzuri, na niliamua kujaribu yote kadri ya uwezo wangu."

Awali Alhamisi, mkuu wa mashindano ya London, Lord Coe, alisema Rudisha "ndiye mwanariadha bora zaidi katika michezo ya mwaka huu".

Rudisha alisema: "Lord Coe ni rafiki yangu mzuri sana, na mapema, mwezi Februari, alinizungusha kuuona uwanja huu. Hilo lilikuwa jambo zuri kwangu. Nilitaka kurudi hapa na kumfanya ajivunie ushindi wangu."