Bacary Sagna ana shaka na Arsenal

Imebadilishwa: 6 Septemba, 2012 - Saa 13:01 GMT
Bacary Sagna

Sagna amesema haelewi ni kwa nini baadhi ya wachezaji mahiri wameruhusiwa kuondoka Arsenal

Mlinzi wa Arsenal, Bacary Sagna, na ambaye pia ni mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa, ameelezea wasiwasi kuhusiana na mipango ya usajili ya klabu.

Timu ya The Gunners imemruhusu Robin van Persie na Alexander Song kuondoka msimu huu wa joto, na mwaka jana iliwaachia wachezaji Cesc Fabregas, Samir Nasri na Gael Clichy kuondoka.

"Mwezi Mei niliitizama timu ya Manchester City katika televisheni wakishangilia ushindi wao. Nilimtizama Samir na Gael wakiliinua kombe. Hilo linakufanya utamani kufanya vivyo hivyo."

"Nilitazamia Robin kuondoka," alisema Sagna, mwenye umri wa miaka 29, alipohojiwa na gazeti la Ufaransa, L'Equipe.

"Lakini nilishangazwa na kuondoka Alex. Ana umri wa miaka 24, na alikuwa na miaka mitatu iliyosalia katika mkataba wake.

"Unapowatizama kati ya wachezaji wawili bora zaidi uliokuwa nao msimu uliopita wakiondoka, basi unaanza kujiuliza maswali."

Mshambulizi Van Persie alinunuliwa na Manchester United baada ya kuelezea kwamba hana nia ya kutia saini mkataba mpya na timu ya Gunners, na Song alielekea Barcelona.

"Mitaani, baadhi ya mashabiki huzungumza nami. Ninaelewa wamekasirika. Mimi ni kama wao, sielewi yote," aliongezea Sagna.

Nasri na Clichy walijiunga na Manchester City mwaka 2011, na kukisaidia klabu kupata ubingwa wa Premier msimu uliopita.

Sagna alijiunga na Arsenal kutoka klabu ya Auxerre mwezi Julai mwaka 2007, na ameichezea Arsenal mechi 205.

Hivi sasa amepumzishwa, kwani bado anaendelea kupona baada ya kuvunjwa mguu katika mechi dhidi ya Norwich mwezi Mei.

Mkataba wake utakwisha mwisho wa msimu wa mwaka 2013-14, na alipoulizwa kama kuna yeyote ambaye ameshauriana naye kuhusiana na mkataba mpya, alisema "La, hakuna yeyote aliyezungumza nami."

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.