Hamilton kuihama McLaren

Imebadilishwa: 6 Septemba, 2012 - Saa 14:00 GMT
Lewis Hamilton

Dereva bingwa wa dunia mwaka 2008 anatazamiwa kujiunga na timu ya Mercedes

Dereva wa Uingereza wa mashindano ya langalanga, Formula One, Lewis Hamilton, yumo katika kukamilisha mipango ya kujinga na timu ya Mercedes msimu ujao.

Habari hizo ni kwa mujibu wa mchambuzi mkuu wa BBC katika masuala ya F1, Eddie Jordan.

Jordan, ambaye zamani alikuwa ni mkuu wa timu, alisema inaelekea Hamilton ataichukua nafasi ya Michael Schumacher, ambaye anatazamiwa kustaafu kwa mara ya pili, mwishoni mwa mwaka huu.

"Ninaamini Hamilton na timu ya Mercedes tayari wameshakubaliana kuhusiana na matakwa ya kibinafsi, na makubaliano rasmi sasa yanatazamiwa," alieleza Jordan.

Kupitia taarifa, Mercedes imeelezea kwamba haina nia ya kuelezea chochote kutokana na uvumi.

Lakini wakaongezea: "Hadi tutakapokuwa katika nafasi ya kuthibitisha kikamilifu juu ya madereva wetu watakaokuwepo msimu ujao, ni wazi kwamba kutakuwa na gumzo kuhusiana na suala hili."

McLaren nao walitoa taarifa yao, wakisisitiza kwamba bado wamo katika mashauri na bingwa huyo wa mwaka 2008 kuhusiana na mkataba mpya.

"Tumearifiwa na kundi la wasimamizi wa Lewis Hamilton kwamba habari hizo sio za kweli," alieleza msemaji wa McLaren.

"Mashauri kati ya Lewis Hamilton na McLaren yanaendelea."

Kampuni inayohusika na maslahi ya Hamilton, XIX Entertainment, pia wanadai kwamba "mashauri yaliyopiga hatua na McLaren kuhusiana na mkataba mpya yanaendelea", na kuelezea kwamba muhimu zaidi sasa ni Hamilton kuangazia mashindano ya mwishoni mwa wiki ya Monza, nchini Italia.

Gumzo limekuwepo kwa muda mrefu kuhusiana na Hamilton, mwenye umri wa miaka 27, kuihama timu ya McLaren, ambayo amekuwa nayo tangu alipokuwa na umri wa miaka 13.

Kampuni inayomsimamia tayari ilifanya mashauri na timu za Red Bull na Ferrari msimu huu wa joto, lakini ikapuuzwa na timu hizo mbili.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.