Kijana Sterling kuichezea England

Imebadilishwa: 10 Septemba, 2012 - Saa 13:57 GMT
Raheem Sterling

Kijana wa Liverpool Raheem Sterling kuichezea timu ya taifa ya England dhidi ya Ukraine

Mchezaji soka wa klabu ya Liverpool mwenye umri wa miaka 17, Raheem Sterling, atashirikishwa katika kikosi cha England ambacho kitapambana na Ukraine katika mechi ya kufuzu ya Kombe la Dunia siku ya Jumanne.

Meneja Roy Hodgson pia amewachukua viungo wa kati Jake Livermore, mwenye umri wa miaka 22, kutoka timu ya Tottenham, na Adam Lallana, mwenye umri wa miaka 24, kutoka klabu ya Southampton.

Mchezaji wa Arsenal, Theo Walcott, hataweza kucheza katika mechi hiyo, kwani anaumwa.

Walcott, pamoja na mchezaji wa Chelsea, Daniel Sturridge, hawakuweza kushiriki katika mazoezi ya timu ya taifa ya Jumatatu asubuhi.

Hata hivyo, Sturridge bado yumo katika kikosi hicho cha timu ya taifa.

Walinzi wa Chelsea, John Terry na Ashley Cole, pia hawatakuwepo katika mechi hiyo ya kundi H, kwani wote wana majeraha ya vifundo vya miguu.

Hodgson alielezea kwamba Walcott anaugua homa, na amerudi katika klabu yake, lakini kuna matumaini Sturridge aliyekuwa na maumivu ya tumbo huenda akawa amepona.

Nahodha Steven Gerrard ameelezea kufurahishwa na hatua ya Sterling kushirikishwa katika timu ya taifa, ambaye msimu huu mara mbili alikuwa kati ya wachezaji 11 wa kwanza kuingia uwanjani katika mechi mbili, na mwishoni mwa msimu uliopita alishirikishwa katika mechi tatu kama mchezaji wa zamu.

“Nadhani anastahili kukaribishwa katika mwito huu. Tofauti aliyoileta kimchezo ni ya kusisimua,” alielezea Gerrard.

"Yeye ni kati ya mwanga wetu unaomulika mno. Muhimu ni kwamba yeye hucheza kwa utulivu. Nadhani haitachukua muda mrefu ubunifu wake kujitokeza kikamilifu."

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.