Mechi ya Mechi

Imebadilishwa: 23 Septemba, 2012 - Saa 00:35 GMT
Liverpool

Liverpool kucheza na Man United ugenini Old Trafford

Meneja wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers, ana nia ya kuwashirikisha wachezaji wake wote mahiri katika pambano kubwa la Jumapili wakati klabu kitakapocheza katika uwanja wa ugenini wa Manchester United, Old Trafford.

Meneja huyo alifanya mabadiliko 11 siku ya Alhamisi, wakati timu yake ilipocheza dhidi ya klabu ya Young Boys, katika mechi ya ligi ya Europa, na kuiwezesha Liverpool kuondoka na ushindi.

Kati ya wachezaji waliopumzishwa wakati huo kwa misingi ya kucheza Old Trafford ni pamoja na Steven Gerrard, Luis Suarez na Joe Allen.

Man United, licha ya kutocheza vizuri sana msimu huu, walifanikiwa kuishinda Galatasaray ya Uturuki usiku wa Jumatano, na mbali na kushindwa na Everton katika mechi yao ya kufungua msimu, wameshinda mechi nyingine zote, licha ya mchezo wao wa kutovutia sana kufikia sasa.

Man U inatazamiwa pia kufanya mabadiliko kidogo katika kikosi ambacho kiliishinda Wigan, na Robin van Persie na Patrice Evra wanatazamiwa kushirikishwa katika pambano hilo la nyumbani.

Kuna mapambano mengi ya ligi kuu ya Premier ambayo mara kwa mara hutajwa kama ya kukata na shoka, lakini kati ya yote hayo, pambano la Jumapili kwa urahisi linapata sifa hizo.

Baadhi ya mashabiki wa soka nchini Uingereza wanasema uhasama kati ya Liverpool na Manchester United ulianza tangu nyakati za ujenzi wa mfereji uliokuza biashara za usafiri wa meli kutoka Liverpool hadi Manchester, na ukaanza kuzua uhasama kuanzia masuala ya kiuchumi hadi muziki, lakini zaidi kupita yote, ikawa ni uadui katika soka. Kwa hiyo, Liverpool inapocheza na Manchester United, basi hiyo ni mechi ya kusisimua sana nchini Uingereza.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.