Mashabiki wa Tottenham washambuliwa Roma

Imebadilishwa: 22 Novemba, 2012 - Saa 16:00 GMT
Tottenham

Mashabiki kumi wa Spurs wamejeruhiwa katika fujo mjini Roma

Idara ya polisi mjini Roma imetangaza kwamba mashabiki kadha wa Tottenham wamejeruhiwa, mmoja wao vibaya mno, kufuatia fujo kuzuka katika baa moja.

Kulingana na taarifa katika vyombo vya habari nchini Italia, wapenda soka hao walishambuliwa na mashabiki wa timu ya kandanda ya nyumbani, Lazio, huku pambano likitazamiwa leo usiku kati ya timu hizo mbili.

Fujo zilitokea mapema alfajiri katika baa moja, katikati ya mji ambako mashabiki wa Spurs walikuwa wakijiburudisha kwa vinywaji.

Maafisa wa polisi walieleza kwamba watu wapatao thelathini, na waliojifunika nyuso zao, huku wakiwa wamebeba vyuma, waliingia moja kwa moja katika baa hiyo.

Mwenye baa hiyo alisema watu hao walivunja dirisha, na kuingia ndani pasipo idhini, na kisha kuwazingira mashabiki wa Spurs, waliojitahidi kujificha.

Lakini fujo ilipoanza, mashabiki kumi wa Tottenham walijeruhiwa.

Taarifa zilizopo ni kwamba mtu aliyeumizwa vibaya mno inaelekea alidungwa kwa kisu.

Watu watano walikamatwa, na wote waliozuiliwa na maafisa wa polisi wa Italia, ni raia wa nchi hiyo.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.