Orodha fupi ya kuwania tuzo ya BBC yatangazwa

Imebadilishwa: 27 Novemba, 2012 - Saa 13:25 GMT
Mo Farah

Mwanariadha Farah ni kati ya watu 12 katika orodha fupi ya wale wanaotazamia kupata tuzo ya BBC ya mwanamichezo bora zaidi mwaka 2012

Orodha fupi ya wanamichezo ambao wanawania tuzo ya BBC ya mwanamichezo bora zaidi mwaka 2012 imetangazwa.

Wengi ya waliotajwa ni wanamichezo walioshinda medali katika michezo ya Olimpiki na Paralimpiki mjini London, mwaka huu wa 2012.

Kati ya wale waliomo kwenye orodha hiyo fupi ya wanamichezo 12 ni pamoja na waendeshaji baiskeli Bradley Wiggins na Sir Chris Hoy, mchezaji tennis Andy Murray, na wanariadha Jessica Ennis na Mo Farah.

Mpiga kasia Katherine Grainger, mchezaji golf Rory McIlroy, bondia Nicola Adams na baharia Ben Ainslie pia wamo katika orodha.

Kwa wale walioshiriki katika michezo ya Paralimpiki, Sarah Storey, Ellie Simmonds na David Weir, pia ni miongoni mwa wanamichezo ambao wana matumaini ya kupata tuzo wakati mshindi atakapotangazwa tarehe 16 Desemba.

Watu watatu walihusika katika kuchagua majina ya wanamichezo katika orodha hiyo fupi, lakini mshindi hasa atachaguliwa na kura ya umma.

Mwaka huu orodha hiyo imetayarishwa na jopo la watalamu wa michezo, kufuatia malalamiko ya namna wanamichezo walichaguliwa mwaka 2011, na orodha ambayo ilikuwa ni wanamichezo wa kiume tu.

Mshindi wa tuzo hilo la BBC mwaka 2000, Sir Steve Redgrave, alishirikiana na Baroness Grey-Thompson, Denise Lewis na Baroness Campbell, mwenyekiti wa UK Sport, pamoja na wawakilishi wengine kutoka magazeti ya Uingereza katika kuwachagua wanamichezo hao katika orodha hiyo fupi.

Umati wa watu 15,000 katika ukumbi wa ExCel, mjini London, unatazamiwa kuwa ndio mkubwa zaidi katika historia ya miaka 59 ya tuzo hiyo.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.