Price amtaka Chisora kwa gharama yoyote

Imebadilishwa: 1 Disemba, 2012 - Saa 00:29 GMT
David Price

Lengo lake ni kupambana na Dereck Chisora

Bondia wa Uingereza David Price amesema angelipenda kuzichapa na Dereck Chisora baada ya pambano dhidi ya Matt Skelton.

Kabla ya pambano la Price na Skelton usiku wa Ijumaa mjini Liverpool, Price alisema ana matumaini kwamba Dereck Chisora ataweza kuipata tena leseni yake ya ndondi kupigana nchini Uingereza, ili waweze kuchapana katika ngumi za uzani wa heavy.

Chisora, mwenye umri wa miaka 28, alipokonywa leseni na bodi inayosimamia ngumi nchini Uingereza, kutokana na utovu wa nidhamu mjini Munich, Ujerumani, katika fujo zilizotokea kati yake na mabondia Vitali Klitschko na David Haye.

"Nadhani ni wazi kwamba ni yeye ninapaswa kupambana naye katika kuutetea ubingwa wangu wa Uingereza, kwani nadhani Dereck ataweza kupigana kwa kiwango kinachostahili cha hadhi ya Uingereza," alisema Price.

Price, mwenye umri wa miaka 29, na ambaye alikuwa atetee mikanda yake ya ubingwa wa Uingereza na Jumuiya ya Madola usiku wa kuamkia Jumamosi mjini Liverpool, amesema hana la kuchagua baada ya kuchapana na Skelton.

"David Haye aliwahi kuwa bingwa wa dunia, na anatamani pambano moja tu, na tunalifahamu [Vitali Klitschko] na Dereck Chisora atapigana kuwania taji la Uingereza, ninaamini hivyo," alisema Price.

Price alipopigana mara ya mwisho mjini Liverpool, kabla ya pambano na Skelton, alimshinda Audley Harrison, kwa kumzima mara moja, kwani pambano lilisimamishwa katika raundi ya kwanza.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.