Eritrea yajiondoa CHAN

Imebadilishwa: 5 Disemba, 2012 - Saa 19:16 GMT
Wachezaji wa soka wa Eritrea

Wachezaji wa soka wa Eritrea wakicheza katika mashindano ya CECAFA

Shirikisho la mchezo wa soka nchini Eritrea limetangaza kuwa halitashiriki katika mechi yao ya kuwania kombe la mataifa bingwa barani Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki katika ligi ya Nyumbani, dhidi ya Ethiopia.

Shirikisho la mchezo wa soka barani Afrika CAF limethibitisha uamuzi huo, lakini halijatoa sababu yoyote ya kujiondoa kwa Eritrea.

Siki ya Jumanne, Shirikisho la mchezo wa soka nchini Ethiopia, liliomba CAF, kupeleka mechi yao na Eritrea katika nchi tofauti, kwa kuwa nchi hizo mbili jirani, zinazozana kuhusu suala la mipaka.

Wachezaji 17 wa timu ya taifa ya Eritrea na daktari wao waliotoweka nchini Uganda siku ya Jumanne, wameomba hifadhi nchini humo.

Kamishna anayehusika na masuala ya wakimbizi katika ofisi ya waziri mkuu, David Apollo Kazungu, ameiambia BBC kuwa wachezaji hao wa Eritrea walimtembelea mapema hii leo kuomba kupewa hifadhi.

Apollo alisema kuwa wachezaji hao na afisa huyo walimueleza kuwa hali nchini mwao sio nzuri na kuwa ofisi yake inachunguza nyaraka zao kabla ya kuchukua hatua.

''wao wote watasalia chini ya serikali ya Uganda kwa kuwa wamesajiliwa rasmi'' aliongeza Bwana Apollo Kazungu.

Kazungu amesema wanashirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi UNHCR, jinsi watakavyowasaidia wachezaji hao wa Eritrea.

Wachezaji wapotea

Pasi ya wachezaji wa soka wa Eritrea

Pasi ya wachezaji wa soka wa Eritrea katika mashindano ya CECAFA

Wachezaji hao hawakurejea katika hoteli walimokuwa wakiishi siku ya Jumapili, baada ya kuondolewa kwenye michuano ya kuwania kombe la taifa bingwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA Senior Challenge mjini Kampala.

Wachezaji watano pekee na maafisa watano wa timu hiyo ndio waliorejea kambini.

Katika mechi zao, Eritrea ilitoka sare za Zanzibar kisha ikapoteza dhidi ya Malawi na Rwanda na hivyo kuondolewa kwenye hatua ya makundi.

Katibu mkuu wa CECAFA Nicolas Musonye amesema ni jambo la kutia moyo kuwa wachezaji hao hatimaye wamejitokeza.

Lakini amesema ni jambo la kusikitisha kuwa wachezaji wa Eritrea wamekuwa na mazoea ya kutoweka katika mashindano kila mwaka.

Mwaka wa 2009 na 2010 wachezaji wengine wa Eritrea pia walitoweka na hatma yao haijulikani.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.