Man City nje ya Uropa

Imebadilishwa: 5 Disemba, 2012 - Saa 10:58 GMT

Wachezaji wa Man City wakati wa mechi yao na Borussia

Manchester City imekosa nafasi ya kushiriki katika ligi ya Uropa baada ya kushindwa bao moja bila jibu, na Borussia Dortmund katika mechi yake ya mwisho kwenye Ligi ya klabu bingwa barani Ulaya.

Ushindi wa Real madrid dhidi ya Ajax ulimaanisha City ingemaliza ya tatu katika kundi D iwapo ingeshinda mabingwa hao wa Ujerumani.

Lakini Dortmund ilionyesha makali yake mapema na kumlazimu mlinda lango wa City, Joe Hart kuokoa misururu ya mashambulizi makali, kabla ya Julian Schieber kufunga bao safi kutokana na pasi la Jakub Blaszczykowski.

Timu hiyo inayofunzwa na Jurgen Klopp tayari ilikuwa imeingia katika raundi ya 16 bora, kama viongozi, na iliwabidi City kujikakamua hasaa Ajax ilipofungwa mapema na Madrid.

City ilipata nafasi chache sana katika dakika 45 za kwanza, na jaribio lake la pekee la kupata bao lilikuwa kupitia mshambulizi Edin Dzeko lakini kipa Roman Weidenfeller, aliuondoa mpira huo nje.

City sasa imebanduliwa kutoka Uropa bila ushindi wowote kutokana na mechi zake sita za makundi. Pointi hizo tatu ilizokusanya ni chache mno ikilinganishwa na tajiriba kubwa ya wachezaji wa kocha Roberto Mancini. Aidha ni chache kabisa kuwahi kupatikana na timu yoyote ya Uingereza katika historia ya miaka ishirini ya mashindano hayo.

Mabingwa hao wa Uingereza watalazimika kuonyesha mchezo bora zaidi watakaporejea uwanjani Jumapili, kukabiliana na mahasimu wa jadi, Manchester United, ambao kwa sasa wanaongoza Ligi kuu nchini Uingereza.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.