Morocco 1 Afrika Kusini 0

Imebadilishwa: 27 Januari, 2013 - Saa 17:25 GMT

Wachezaji wa Afrika Kusini


Timu za kundi A zinakamilisha michezo yao leo kwa kucheza mchezo wa tatu na wa mwisho kwa kila timu ya kundi hilo.

Afrika Kusini yenye pointi 4 itakuwa inamenyana na Morocco yenye pointi 2 kuwania nafasi ya kucheza robo fainali.

Cape Verde yenye pointi 2 pia itakuwa ikionyeshana kazi na Angola yenye pointi 1.

Kila timu inaweza kufuzu kucheza robo fainali ili mradi iweze kushinda mechi yake.

Angola itabidi ipiganie kushinda kwa idadi kubwa ya magoli, kwani hata ikishinda mechi yake dhidi ya Cape Verde itaishia kupata pointi nne ambazo tayari Afrika Kusini inazo.

Kwa hesabu hizo nafasi ya Angola ni finyu zaidi kulinganisha na timu nyingine za kundi hilo kufuzu kucheza robo fainali.

Manucho mchezaji wa Angola

Bafana Bafana kuwika nyumbani?

Kila kundi litatoa timu mbili, hivyo timu nane ndizo zitakazoingia robo fainali kutoka makundi manne yaliyopo yenye timu nne kila moja.

Michezo yote miwili ya kundi hili itachezwa kwa wakati mmoja ili kuepuka kupanga matokeo.

Timu ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, wenyeji wa michuano hii, wanaingia katika viwanja wakiwa na kundi la mashabiki nyuma yao wakiwahamasisha kushinda. Mwaka 1996 ilipoandaa mashindano kama haya iliweza kuibuka mabingwa.

Je, timu hiyo itarudia historia hiyo? Wachambuzi wa masuala ya michezo wanasema itakuwa vigumu sana kwa Afrika Kusini kurejelea historia hiyo kutokana na aina ya wachezaji ilionao sasa wakilinganishwa na kikosi cha mwaka 1996 enzi za kina Mark Fish, Lucas Radebe na Doctor Khumalo.

Mchezaji mwenye kiwango cha wachezaji hao kwa timu ya sasa ya Bafana Bafana ni Siphiwe Tshabalala.

Kikosi hicho kiko chini ya kocha Gordon Igesund, ambaye ameichukua timu hiyo muda mfupi kabla ya kuanza kwa michuano ya Afcon.

Hiyo ni changamoto kubwa kwake kuiwezesha timu hiyo kutwaa kombe hilo.

Kwa upande wa Angola haina umaarufu sana katika michuano ya Kombe la Afrika, lakini lazima ikumbukwe kuwa katika miaka ya 2008 na 2010, nchi hiyo imeweza kufikia kiwango kizuri kwa kucheza hatua ya robo fainali.


Mchezaji ambaye Cape Verde itapaswa kumchunga katika mchezo wa leo dhidi ya Angola ni Manucho mchezaji wa timu ya Real Valladolid, ambaye ana uwezo mkubwa wa kimataifa katika kupachika magoli.

Na kwa upande wa Morocco ni timu ambayo ni miongoni mwa vigogo wa soka barani Afrika na katika michuano hiyo ya Mataifa Bingwa wa Kombe la Afrika.

Wachezaji hatari wa Morocco

Marouane Chamakh mchezaji wa Morocco

Wachezaji nyota wa timu hiyo ya Simba wa Atlas ni pamoja na Marouane Chamakh, mwenye umri wa miaka 28 anayechezea klabu ya Arsenal ya England.

Hata hivyo amekuwa ni mshambuliaji zaidi kuliko kuwa mpachika magoli.

Pamoja na mlinda mlango Nadir Lamyaghri, sehemu ya ulinzi ya Morocco si imara sana, kutokana na kukosa wachezaji wenye uzoefu.

Hata hivyo mchezaji Mehdi Benatia wa klabu ya Udinese, ni mtu wa kuchungwa.

Hadhi ya Cape Verde imeimarika katika miaka ya karibuni.

Ni nchi yenye wachezaji wenye vipaji. Mathalani mchezaji maarufu wa Ufaransa, Patrick Vieira, baba yake ni mtu wa kutoka Cape Verde, huku nyota wa Sweden Henrik Larsson, mama yake ni mtu wa Cape Verde, lakini visiwa hivyo havina umaarufu sana katika soka barani Afrika.

Michuano ya mwaka 2013 ni ya kwanza kwa timu hiyo kufuzu kucheza.

Hata hivyo kiwango chao cha uchezaji kimekua na hiyo kimedhihirika katika hatua ya kuwania kufuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika.

Pia katika fainali hizo zinazoendelea nchini Afrika Kusini, Cape Verde imeonyesha ushindani mkubwa.

Kwa hiyo huenda ikawa inalenga mbali zaidi kwa kutaka kufuzu kucheza hatua ya robo fainali.

Na iwapo itaibwaga Angola itakuwa na pointi tano, huku ikiomba Afrika Kusini iibwage Morocco au itoke sare nayo.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.