Kundi C kibaruani kusaka pointi muhimu

Image caption Kikosi cha Burkina Faso

Timu za kundi C leo zinarejea tean uwanjanu kusaka pointi tatu muhimu kutafuta nafasi ya kucheza robo fainali ya michuano ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini.

Vinara wa kundi hilo Burkina Faso yenye pointi 4 itapamabana na mabingwa watetezi Zambia ambayo ina alama mbili.

Timu nyingine za kundi hilo ni Ethiopia yenye pointi 1 na leo inacheza na Nigeria ambayo kufikia sasa imejizolea alama mbili.

Kwa kuwa timu hizo zote zina nafasi ya kufuzu kwa robo fainali, cechi hizo zote zitachezwa kwa wakati mmoja.

Burkina Faso, kwa mara ya kwanza ilicheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1978, wakati huo ikijulikana kama Upper Volta na walitolewa katika hatua za mwanzo tu za michuano hiyo.

Image caption Mabingwa watetezi, timu ya Zambia

Ilipita miaka 18, timu hiyo iliposhiriki kwa mara ya pili mwaka 1996, wakati mashindano hayo yalipoandaliwa nchini Afrika Kusini. Pia wakati huo walitolewa katika hatua ya makundi.

Miaka miwili baadaye walipoandaa michuano hiyo ilimaliza katika nafasi ya nne, yakiwa ni mafanikio makubwa zaidi kufikiwa na timu hiyo.

Wachezaji wengi wa Burkina Faso wanacheza nje ya nchi, hususan Ufaransa.

Nao mabingwa watetezi Zambia itabidi wakaze musuli, kwani wakishindwa katika mchezo wake na Burkina Faso tayari watakuwa wamepoteza kombe hilo waliloshinda mwaka uliopita.

Nigeria iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa katika michuano ya mwaka huu haikuonyesha makeke yaliyotarajiwa kutoka vijana hawa wa Super Eagles.

Kwa hiyo bado wana mlima mrefu watakapopambana na Ethiopia ambayo haitapenda kurudi Addis Ababa mapema. Ushindi utawanusuru na kuangalia matokeo ya Zambia na Burkina Faso.