Jahazi la Mali lazidi kuzama

Image caption Wachezaji wa Nigeria

Nigeria inaoongoza kwa magoli 4-1 dhidi ya Mali, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa nusu fainali za Kombe la Afrika.

Elderson Echiejile amefunga magoli mawili katika dakika ya 25 na 30.

Goli la tatu limefungwa na Emenike katika dakika ya 44 baada ya mpira aliopiga kumgonga Momo Sissoko wa Mali.

Kipindi cha kwanza kimemalizika na sasa ni mapumziko, Nigeria ikiongoza kwa magoli 3-0.

Ahmed Musa amezidi kufifisha matumaini ya Mali kucheza fainali baada ya kupachika goli la nne dakika ya 60.

Mali haijaonyesha kukata taama japo muda unazidi kuyoyoma, kwani katika dakika ya 70 Cheikh Diarra ameifungia bao timu yake.

Nigeria kuingia nusu fainali waliwabwaga Ivory Coast, timu ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kucheza fainali kutokana na ubora wa wachezaji wake.

Katika mchezo na Ivory Coast, Nigeria walishinda magali 2-1.

Nayo Mali iliwatoa wenyeji wa mashindano Afrika Kusini kwa njia ya mikwaju ya penalti 3-1 baada ya timu hizo kucheza dakika 120 zikiwa zimefungana goli 1-1.

Timu nyingine katika nusu fainali za Afcon ni Ghana itakayokwaruzana na Burkina Faso. Ghana waliitoa Cape Verde katika hatua ya robo fainali kwa magoli 2-0, huku Burkina Faso wakiifunga Togo kwa goli 1-0.

Timu ya Nigeria inawategemea wachezaji wake kadhaa kutoka nje kama vile Victor Moses na Obi Mikel wanaocheza ligi kuu ya England.

Nayo Mali ina wacheza kadhaa maarufu katika ligi mbalimbali za dunia akiwemo Seydou anayechezea timu ya Dalian Aerbin nchini Uchina na Momo Sissoko.