Man City yaadhibiwa na Southampton

Image caption Wachezaji wa Southampton

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Premier ya England, Manchester City wamenyolewa bila maji na Southampton kwa kunyukwa magoli matatu kwa moja katika mchuano mkali wa ligi kuu ya Premier.

Jason Puncheon aliifungia Southampton bao lake la kwanza kabla ya Steven David kuongeza la pili.

Lakini mabingwa hao watetezi walifufua matumaini yao kwa kufunga bao la pili kupitia kwa nyota wake Edin Dzeko.

Lakini vijana hao wa Southampton ambao wanashiriki katika ligi hiyo kwa mara ya kwanza, baada ya kupandishwa daraja msimu uliopita, walijiimarisha na kufunga bao la tatu baada ya mcheza kiungo wa Manchester City Gareth Barry kujifunga.

Juhudi za mabingwa hao watetezi za kusawazisha ziligonga mwamba pale wachezaji wa Southampton walipoendeleza mashambulio yao dhidi ya Manchester City.

Kufuatia ushindi huo muhimu, Southampton sasa imepanda hadi nafasi ya kumi na saba na alama 27, huku Manchester City ikisalia katika nafasi ya pili na alama hamsini na tatu alama tisa nyuma ya Manchester United ambayo bado ingali na mechi moja zaidi.

Katika mechi zingine Tottenham imeishinda Newcastle kwa magoli mawili kwa moja Norwich ikatoka sare ya kutofungana bao lolote na Fulham, Stoke city nayo ikaishinda Reading kwa mabao mawili kwa moja na Swansea ikainyesha QPR magoli manne kwa moja.