Real Madrid,Manchester United sare

Image caption Christiano Ronaldo wa Real Madrid

Real Madrid ya Hispania na Manchester United ya England zimetoka sare baada ya kufungana bao moja kwa moja katika mchezo wa mabingwa barani Ulaya, UEFA, uliochezwa katika uwanja wa Real Madrid, Bernabeau.

Manchester United United ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufunga goli katika dakika ya 20 ya mchezo, baada ya Danny Welbeck kufunga kwa kichwa mpira wa Kona. Hata hivyo furaha ya Manchester United ilidumu kwa dakika kumi tu, kwani katika dakika ya 30 Christian Ronaldo iliisawazishia timu yake goli alilofunga kwa kichwa baada ya mpira wa adhabu ndogo.

Baada ya hapo timu zote ziliendelea kushambuliana hadi mapumziko, huku Real Madrid ndiyo ikitawala zaidi mpira na Manchester United ikifanya mashambulio ya kushtukiza.

Kipindi cha pili kilianza kwa Manchester United kushambulia lango la Real Madrid, hata hivyo mashambulio yaliigeukia Manchester United, huku mlinda mlango wake David de Gea akiokoa michomo mingi kutoka kwa vijana wa Real Madrid.

Image caption Danny Welbeck mfungaji wa goli la Man U

Manchester United ilikuwa na bahati kupona kipigo kutoka kwa vijana wa Mourinho, kutokana na kuumiliki mpira muda mrefu na kupeleka mashambulio ya mara kwa mara kiasi kwamba D e Gea alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo hiyo.

Alipoulizwa Mourinho kuhusu mpambano huo, anasema vijana wake walitawala mchezo huo, huku wapinzani wao wakisubiri kufanya mashambuliuo ya kushtukiza. Na kwa upande wa kumiliki mpira, Mourinho alisema timu zote zilicheza asilimia 50 kwa 50.

Hata hivyo kwa mujibu wa takwimu za mchezo huo, Real Madrid ilitawala kwa asilimia 54 dhidi ya 46.

Katika mchezo mwingine wa michuano hiyo, Shakhtar Donetsk ya Ukraine imetoka sare ya 2-2 na Borussia Dortmund ya Ujerumani.