Beniteza akanusha mzozo na wachezaji

Image caption Rafael Benitez

Kaimu kocha wa Chelsea Rafael Benitez amesisitiza kuwa ana uhusiano mwema na wachezaji wote wa klabu hiyo na kuwa anaungwa mkono na wote.

Ripoti zinasema kuwa Benitez mwenye umri wa miaka, 52, alizozana vikali na baadhi wa wachezaji wake, baada ya kulazwa magoli mawili kwa bila na Manchester City siku ya Jumapili.

''Ninaweza kutoa thibitisha kuwa wachezaji wote wanafahamu kile tunachojaribu kufanya na ninaamini yale ninayoyatenda'' Alisema kocha huyo.

'' Wachezaji wote wanaunga mkono mawazo na mapendekezo yetu kwa asilimia mia moja'' Aliongeza Benitez.

Image caption John Terry Nahodha wa Chelsea

Chelsea imeshinda mechi kumi na tatu kati ya mechi 26 walizocheza chini ya Benitez ambaye aliteuliwa mwezi Novemba mwaka uliopita na kwa sasa inashikilia nmafasi ya nne kwenye msururu wa ligi kuu ya premier, alama kumi na tisa nyuma ya vinara wa ligi hiyo kwa sasa Manchester United.

Hata hivyo kocha huyo kutoka Uhispania anasema kuwa wachezaji wake wana uhakika wa kumaliza katika nafasi za tatu bora kwenye ligi hiyo.

Mwaka uliopita, Chelsea ilimaliza katika nafasi ya sita na Benitez anaseka kikosi cha sasa ni bora zaidi.

Chelsea ambayo ilishindwa katika nusu fainali ya kuwania kombe la ligi na Swansea inachuana na Middlesbrough, katika mechi ya raundi ya tano ya kuwania kombe la FA Jumatano usiku.

Nahodha wa Chelsea John Terry, ambaye mapema mwezi huu alikanusha madai ya kuwepo kwa uhasama kati yake na Benitez, amesemekana kuzozana na kocha huyo.