Je Man United itawika bila RVP?

Image caption Robin Van Persie na Nyota wa Real Madrid Christiano Ronaldo

Aliyekuwa mcheza kiungo wa Manchester United Quinton Fortune, ana matumaini makubwa kuwa klabu yake ya zamani inaweza kuishinda Real Madrid hata bila kuwepo kwa nyota wake Robin van Persie.

Van Persie kwa sasa anauguza jeraha la kiuno, lakini anatarajiwa kuwa sawa wakati wa mechi ya marudiano katika uwanja wa Old Trafford, ambayo Manchester United ni sharti ishinde baada ya kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja katika mechi yao ya raundi ya kwanza.

"itakuwa pigo kubwa kwa Man United ikiwa Robin van Persie hatashinda, lakini jambo kuu ni kuwa ni suala la wachezaji wote kwa pamoja'' Fortune, aliliambia BBC.

" Naamini ni wakati wa Manchester United. Wachezaji wake kwa sasa wana hamu ya kushinda'' Alisema mchezaji huyo wa zamani.

Image caption Quinton Fortune

Van Persie amefunga jumla ya magoli 23 katika msimu wake wa kwanza na United katika ligi kuu zikiwemo tatu katika michuano ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya.

Hata hivyo United ilipata pigo pale, Van Persie alipopata jeraha na kiuno wakati wa mechi ya na QPR siku ya Jumamosi, mechi ambayo walishinda kwa mabao mawili kwa bila.

Huenda mchezaji huyo asijumuishwe katika mechi yao ya siku ya jumamosi dhidi ya Norwich, ili kuumpa nafasi zaidi ya kupona, lakini kocha wake Sir Alex Ferguson, anatarajia kuwa atakuwa tayari kwa mechi hiyo dhidi ya mabingwa wa Uhispania.

Phil Jones, ambaye alionyesha mchezo mzuri katika safu ya ulinzi wakati wa mechi ya raundi ya kwanza, vile vile anauguza jeraha na mguu.

Fortune ameongeza kuwa mchezaji mwingine ambaye anaendelea kuimarika na ambaye anaendelea kujikita kama mchezaji wa kutegemewa katika kikosi hicho cha Manchester United ni Michael Carrick.