Hodgson kufikiria kumuita tena Ferdnand

Ferdinand
Image caption Rio Ferdinand akiitumikia England

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya England,Roy Hodgson amesema atasubiri kuona kama ataweza kumuita kwa mara nyingine beki wa Manchster United Rio Ferdinand.

Kocha huyo amesema alijisikia vibaya kuona Ferdinand akijiondoa kwenye timu ya taifa ya England baada ya kumuita kwaajili ya michezo ya kusaka tiketi ya kushiriki kombe la dunia dhidi ya visiwa vya San Marino na Mentengro.

Ferdinand ambaye alijiondoa kwenye kikosi hicho cha Uingereza kwa sababu za kuwa alikwishajipangia ratiba maalumu kwaajili ya kuuguza majeraha yake katika kipindi hiki ambacho klabu yake itakuwa haina mechi zozote kwa zaidi ya wiki moja.

Nyota huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 34,amekwishaicheza Uingereza michezo 81 na tayari yupo nchini Qatar tayari kwaajili ya kuwa mchambuzi kwenye mechi kati ya Uingereza na San Marino Ijumaa hii.

Hata hivyo kocha Hodgson akijibu swali kuhusiana na Ferdinand kusafiri hadi Qatar kuchambua mechi ambayo angekuwa uwanjani akicheza,alisema hakuwa na wazo lolote,lakini amejisikia vibaya kuona beki huyo hajajiunga na timu yake na kusafiri kwake kwenda Qatar ni matakwa yake binafsi na klabu yake.

Mechi ya mwisho Ferdinand kuichezea England ilikuwa dhidi ya Uswis mwezi Juni mwaka 2011,Alikosa fainal za mataifa barani Ulaya mwaka 2012 ambapo kocha Roy Hodgson alisema ameacha kumuita nyota huyo kwa sababu za Kimpira.

Hivi sasa Hodgson itamlazimu kumchagua beki wa Manchester City Jeleon Lescott, Chris Smalling wa Manchester United ama Steven Caulker wa Tottenham au Steven Taylor wa Newcastle United kwenye safu ya ulinzi itakayocheza na visiwa vya San Marino Ijumaa hii katika mchezo wa kundi H kusaka tiketi ya kushiriki kombe la dunia mwakani nchini Brazil.

HISTORIA YA FERDINAND TIMU YA TAIFA.

•1997: Alicheza mechi ya kwanza dhidi Cameroon kwenye uwanja wa Wembley •1998: Alikuwa kikosi kilichoshiriki kombe la dunia. •2000: Aliachwa kwenye kikosi kilichoshiriki kombe la mataifa ya Ulaya. •2002: Alifunga bao lake kwanza akiwa katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Denmark katika michuano ya kombe la Dunia. •2004: Alifungiwa miezi nane kwa kushindwa kufanya vipimo vya madawa ya kuongeza nguvu michezoni. •2006: Alicheza mechi tano za kombe la dunia nchini Ujerumani. •2008: Alivaa kitambaa cha Unahodha kuiongoza England katika mechi ambayo walipoteza dhidi ya Ufaransa. •2010: John Terry anavuliwa unahodha na Ferdnand alipewa,lakini kutokana na majeruhi alishindwa kushiriki Michuano ya kombe la dunia. •2011: Alitimiza mechi yake ya 81 wakati England ilipocheza dhidi ya Uswis katika mechi ya kufuzu kombe la mataifa barani Ulaya.