Suarez kusalia Liverpool

Suarez
Image caption Suarez akishangilia moja ya mabao yake

Mkurugenzi Mtendaji wa klabu ya Liverpool ya nchini Uingereza Ian Ayre amethibitisha mshambuliaji wa klabu hiyo Luis Suarez ataendelea kuitumikia timu hiyo.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa mwenye umri wa miaka 26 kutoka Uruguay,alinukuliwa siku za karibuni akisema atafikiria kuhusu kuihama Liverpool iwapo timu inayoshiriki michuano ya kombe la Klabu bingwa barani Ulaya ingehitaji huduma yake,lakini Ian ameiambia BBC kuwa mchezaji huyo ataendelea kuvaa jezi nyekundu za majogoo wa Anfield msimu ujao.

Ian,ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na BBC Radio 5 mapema alhamis asubuhi,ambapo amesema ana uhakika wa kumbakisha nyota huyo anayeongoza kwa upachikaji mabao kwenye ligi kuu nchini England,huku akiongeza kuwa huenda waandishi wa habari walikosea kumnukuu Suarez ambaye lafudhi yake ya lugha ya Kiingereza siyo nzuri.

Suarez alisajiliwa na Liverpool kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni 22.7 mwezi Januari mwaka 2011 na amekwishaifungia Liverpool jumla ya mabao 29 msimu huu yakiwemo mabao 22 kwenye ligi kuu soka nchini England.

Suarez Mfungaji

Liverpool mpaka sasa bado haijafanikiwa kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya tangu Suarez ajiunge na timu hiyo na harakati zao za kushiriki michuano hiyo msimu ujao zinaonekana kuwa ngumu kutokana na mwenendo wa timu hiyo kwenye ligi kuu ya England ambapo hivi sasa wanakamata nafasi ya saba wakiwa na pointi 45.

Mapema mwaka huu,Luis Suarez alinukuliwa na gazeti la nyumbani kwao Uruguay kuwa,iwapo itakuja timu nyingine itakayokuwa ikishiriki kwenye michuano ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya,angefikiria upya kuihama klabu yake ya Liverpool,lakini Mkurugenzi wa Liverpool Ian Ayre amesema Suarez ana mkataba wa miaka minne ambao aliuongeza kwenye majira ya joto msimu uliopita,hivyo ana uhakika mchezaji huyo hataondoka Anfield.

Desemba mwaka jana,Suarez alifungiwa kutocheza mechi nane za ligi kuu soka nchini Uingereza na chama cha soka nchini Uingereza kwa kosa la ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji wa Manchester United Patrice Evra.

Image caption Mshambuliaji wa Liverpool,Luis Suarez

WASIFU WA SUAREZ.

Jina:Luis Alberto Suárez Díaz

Kuzaliwa: 24/1/1987.

Klabu alizopitia: Nacional,Groningen,Ajax,Liverpool

Mechi alizocheza Liverpool: 92.

Mabao aliyofunga Liverpool: 50