Vettel ashinda Malaysian GP

Sebastian Vettel
Image caption Sebastian Vettel akishangilia

Bingwa mtetezi wa mashindano ya mbio za magari ya Langalanga Sebastian Vettel ameshinda mbio za Malaysia Grand Prix licha ya kukaidi maagizo ya mabosi wake kampuni ya Red Bull.

Vettel ambaye ameshinda mbio hizo mbele ya dereva mwenzake Mark Weber ambaye alikuwa akiongoza baada ya kituo cha mwisho,licha ya kupewa maagizo na mkuu wa Red Bull ya kukaa nyuma ili kumpisha Webber alionekana kufanya vizuri toka kuanza kwa mbio hizo zilizofanyika hii leo huko nchini Malaysia.

Baada ya ushindi huo,Bosi wa Red Bull alisikika akimpongeza Vettel,lakini akimwambia ana kazi ya kujieleza zaidi kwa nini amekiuka maagizo ya Timu yake na kuanza kushindana na Dereva mwenzake kutoka Timu ya Red Bull.

Sebastian Vettel mwenyewe ameomba radhi kwa kitendo hicho,huku akisema alikuwa hana jinsi kwani wote walikuwa wakishindana kushinda.

Dereva Muingereza Lewis Hamilton alimaliza wa tatu mbele ya Nico Roseberg wa Timu yake ya Mercedes licha ya kujisahau na kusimama kwenye kituo kisicho kuwa chake kubadilisha matairi ya gari kwenye raundi ya mwisho ya mbio hizo.

Malaysian Grand Prix hii leo zilikuwa mbio zenye msisimko mkubwa kwani,licha ya tukio la kushindania nafasi ya kwanza kati ya Mark Webber na Sebastian Vettel, Pia Lewis Hamilton na Nico Roseberg wa Mercedes walikuwa kwenye kilinge cha kugombea nafasi ya pili ambapo Nico Roseberg aliambiwa ampishe Hamilton ambaye alionekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuipa ushindi kampuni yake mpya.

Utata wa kugombea nafasi ya kwanza kati ya Sebastian Vettel na dereva mwenzake Mark Webber ulianza siku nyingi ambapo kwenye mbio za mwaka 2010 za nchini Uturuki,magwiji hao wa langalanga waliwahi kutaka kuleta maafa baada ya kugombea nafasi ya kwanza kumaliza kwenye raundi ya mwisho.

Mark Webber ameendelea kulalamika kwa kusema anajua uongozi wa kampuni yao utaendelea kuwa upande wa Vettel licha ya kukaidi maagizo yao kwa mara nyingine,tabia ambayo Webber ameilalamikia kwa muda mrefu.

Wakati huo huo,Dereva wa magari ya kampuni ya Ferari,Fernando Alonso alishindwa kumaliza mbio hizo baada ya gari lake kupata ajali kwa kugongana na gari la Sebastian Vettel wakati akitoka kwenye kituo cha kuweka mafuta.

Matokeo haya ya leo yanamuweka Vettel kileleni mwa msimamo wa mbio za Formula One kwa zaidi ya point 11 nyuma ya Kimi Raikkonen wa kampuni ya Lotus ambaye kwenye mbio za leo alimaliza wa saba.

MATOKEO YA MALAYSIAN GP