Ligi kuu England yachacha

Man.Utd yazidi kuongoza
Image caption Tamaa ya kuweka rekodi

Klabu ya Manchester United imezidi kupiga hatua ya kushinda taji lake kwa mara ya 20 kwa ushindi mwepesi wa bao 1-0 dhidi ya Sunderland.

Bao la United lilipatikana katika kipindi cha kwanza kupitia mkwaju wa Van Persie uliokua ukielekea nje na kumgonga beki wa Sunderland Titus Bramble na kuishia kimyani. Ushindi huu unaimarisha uongozi wa Man.United kileleni ikiwa na pointi 77.

Nyuma yake ni klabu inayotetea taji hili la Ligi kuu ya England, Manchester City ikiwa nyuma kwa pointi 15 kufuatia ushindi wake wa bao 4 -0 dhidi ya Newcastle United kwenye uwanja wa Etihad.

Carlos Tevez alifunga bao la City la kwanza kabla ya David Silva kuongezea la pili. Man City ilionyesha nguvu ya ziada katika kipindi cha pili, na Vincent ambaye kwa mda amekua nje ya michuano akiuguza jeraha alipenyeza pasi ya Gareth Barry kuhesabu la tatu na Yaya Toure kuhitimisha kwa mkwaju baada ya golikipa kuutema mpira.

Image caption Spurs yapanda hadi 3 bora

Tottenham ilipanda hadi nafasi ya tatu kwa ushindi wa ugenini dhidi ya Swansea kwenye uwanja wa ''Liberty Stadium.''

Baada ya vichapo viwili, safari hii Spurs ilitaka ianze mapema na kupitia Jan Vertonghen aliyeshirikiana vizuri na Gareth Bale alifunga bao baridi mapema katika kipindi cha kwanza. Mchezaji huyo baadaye alimuona Bale na kumpelekea pasi ambayo hata golikipa alibaki ameduwaa kwa jinsi mpira ulivyopigwa kutoka umbali wa yadi 20.

Bahati mbaya ya Swansea ilionekana pale gonga ya kichwa cha Nathan Dyer ilipogonga mwamba na kumgusa kabla ya kutoka nje. Ni baada ya kuhudi kali ambapo mshambuliaji Michu aliweza kupenya na baada ya kugonga mwamba mpira uliishia wavuni. Hata hivyo Swansea haikuweza kupata bao na kuiachia Spurs pointi zote tatu na nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi kuu ya England.

Nafasi hiyo ya tatu ilitazamiwa kuwa ya Chelsea ikicheza ugenini dhidi ya klabu inayotishiwa kushuka daraja, Southampton. Matumaini ya Chelsea yalididimia kwa mabao mawili ya Jay Rodriguez na Rickie Lambert.

John Terry alijitahidi na kuipatia Chelsea bao la kichwa lakini nia ya Southampton ulikua ushindi ndipo Rickie Lambert alipofunga bao la free kick kutoka umbali wa yadi 25 na kuiacha Chelsea ikishuka kutoka nafasi ya tatu na kulala katika nafasi ya nne.

Arsenal inayotizama nafasi hizo nne kwa tamaa kubwa iliikaribisha klabu ya Reading iliyobadili Kocha hivi karibuni na katika kipindi cha kwanza ambapo mshambuliaji Yao Gervinho alikubali mpira kutoka kwa Santi Cazorla na kufunga bao la Arsenal.

Arsenal ilizidi kudhibiti mchezo huu na baada ya mapumziko Cazorla akafunga bao la kuupinda mpira ulioishia wavuni kabla ya Olivier Giroud kuongezea la tatu. Hata hivo Reading ilipunguza wingi wa magoli kupitia Hal Robson-Kanu, lakini Mikel Arteta alithibitisha ushindi unabaki uwanja wa Emirates kwa kufunga mkwaju wa peneti baada ya Alex Oxlade-Chamberlain kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari.

Mashariki mwa jiji la London klabu ya West Ham iliondoa wasiwasi wa mashabiki wa uwezekano wa klabu yao kushuka daraja kwa kuichapa vizuri West Brom 3-1.

Klabu ya Wigan iliweza kupanda kutoka eneo la hatari kwa ushindi mfinyu wa bao 1-0 dhidi ya Norwich City kupitia mshambuliaji Arouna Kone kwenye uwanja wa DW Stadium.