Man City yaitandika Man United 2-1

Wachezaji wa Manchester City wakishangilia
Image caption Wachezaji wa Manchester City wakishangilia

Mabingwa watetezi wa taji la ligi kuu soka nchini England Manchester City,wameendelea kuwa na matumaini ya kutetea taji lao baada ya kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani zao wa jadi Manchester United kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Old Traford.

City ndio walikuwa wa kwanza kupata bao lao kupitia kwa James Milner kwa shuti la wastani baada ya makosa ya Ryan Gigs ambaye aliupoteza mpira ulio zaa bao hilo kunako dakika ya 51 ya mchezo.

Haikuwachukua muda mrefu United,kwani kunako dakika ya 59,United ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Phil Jones kwa kichwa baada ya mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa na Robin Van Persie na mpira huo kumgusa mgongoni nahodha wa Manchester City,Vincent Kompany.

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye uwanja wa Old Traford,nyumbani kwa Manchester United,Ilishuhudia United wakionekana kuelemewa kimbinu na Man City ambao baada ya mabadiliko waliyoyafanya kwa kumtoa Samir Nasri na kumuingiza Sergio Aguero,Yalizaa matunda baada ya Muanjentina Sergio Aguero kuifungia timu yake bao la pili na la ushindi kwenye dakika ya 78,bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo huo.

Manchester City inakuwa timu ya pili kuifunga Manchester United nyumbani kwenye mechi za ligi kuu msimu huu baada ya Tottenham Hotspurs kufanya hivyo mwezi Desemba mwaka jana.

Licha ya kufungwa,United itaendelea kuongoza ligi kuu ya England ikiwa na tofauti ya point 12 na Manchester City ambao wanakamata nafasi ya pili.

Mechi ijayo Manchester United itacheza na Stoke City siku ya jumamosi wakati Manchester City itasafiri hadi jijini London kucheza na Chelsea kwenye mchezo wa nusu fainali ya Michuano ya kombe la FA.