Usiku wa Ulaya wamalizika kwa maajabu

Image caption Cristiano Ronaldo akishangilia bao la pili

Mabingwa wa mara tisa wa michuano ya kombe la Klabu bingwa barani Ulaya,Real Madrid licha ya kufungwa mabao 3-2 na Galatasaray ya Uturuki,wamefanikiwa kufuzu hatua inayofuata ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya na kuandika rekodi ya kuwa timu iliyofika mara nyingi hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Madrid ambayo hii ni mara yao ya 24 kutinga hatua ya nusu fainali,walianza kwa kupata bao la kuongoza ugenini kupitia kwa Cristiano Ronaldo aliyefunga bao hilo dakika ya saba ya mchezo na kumfanya kuwa na magoli kumi kwenye michuano hiyo msimu hu.

Galatasaray walisawazisha bao hilo kipindi cha pili kunako dakika ya 58 kupitia kwa beki wa kimataifa wa Ivory Cost,Emmanuel Eboue aliyemalizia pasi ya Wesley Sneijder na kufungwa bao maridadi kwa shuti la kiufundi

Bao hilo lilionekana kuwachanganya vijana wa Jose Mourinho kwani,dakika ya 70 na 72 walijikuta wakifungwa mabao mawili ndani ya dakika mbili mfululizo,mabao yaliyofungwa na kiungo wa zamani wa Inter Milan aliyehamia Galatasaray msimu huu Wesley Sneijder na Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na nahodha wa timu ya taifa Ivory Cost,Didier Drogba.

Huku Gala wakiwa wanaendelea kulisakama lango la Madrid,beki mkongwe wa timu Hispania na Real Madrid, Alvaro Arbeloa alizadiwa kadi nyekundu kwa kutumia lugha isiyo ya kiungwana baada ya kucheza ndivyo sivyo.

Pamoja na kucheza pungufu,Madrid waliendelea kumudu mchezo huo na ikiwa imebakia dakika moja mchezo kumalizika Cristiano Ronaldo aliipatia timu yake bao la pili na bao lake la 11 kwenye michuano hiyo msimu huu na pia goli lake la 21 kwenye michezo 20 ya klabu bingwa toka msimu wa 2011/12.

Hadi mchezo unamalizika Galatasaray 3-2 Real Madrid,lakini Madrid wamefuzu kwa jumla ya mabao 5-3 baada ya ushindi wa 3-0 nyumbani wiki iliyopita.

Matokeo hayo yanawafanya Madrid kutangulia katika nusu fainal ya Michuano ya klabu bingwa barani Ulaya ambapo kuna uwezekano kocha wake Jose Mourinho akaandika rekodi ya kipekee kuwa kocha wa kwanza kushinda mataji matatu ya Klabu barani Ulaya na vilabu vitatu tofauti baada ya kufanya hivyo akiwa na FC Porto ya Ureno mwaka 2004 baada ya kuwafunga AS Monaco kwa mabao 3-0 na kisha baadaye mwaka 2010 alipokuwa kocha wa Inter Milan ya Italia katika mchezo ambao Inter iliwafunga 2-0 Bayern Munich ya Ujerumani.

Katika Mchezo mwingine, Borussia Dortmund ya Ujerumani nayo imetangulia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya ushindi wa 3-2 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Signal Iduna Park dhidi ya Malaga ya Hispania.

Mchezo huo ambao ulikuwa na kila aina burudani,ulikumbusha mechi ya fainali ya Manchester United na Bayern Munich mwaka 1999 kwa kupatikana mabao mawili ya haraka ndani ya dakika nne za nyongeza kabla ya mchezo kumalizika.

Dortmund walianza kufungwa bao la mapema dakika ya 25 lakini walizinduka na kusawazisha bao hilo kupitia kwa Roberto Lewandowski kunako dakika ya 40 ya mchezo.

Malaga walipata bao la pili dakika ya 82 kupitia kwa Eliseu Pereira Dos Santo na kuwafanya mashabiki wa Dortmund kuwa wanyonge hasa wakiwa na kumbukumbu ya kulipoteza kombe la ligi kuu ya Ujerumani wikiendi iliyopita kwa kushuudia Bayern Munich wakitawazwa kuwa mabingwa wapya.

Dakika tatu kabla ya Mchezo kumalizika wakiwa kwenye muda wa nyongeza, Dortmund walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Marko Reus na baadaye ikiwa imesalia dakika moja Mbrazil Felipe Augusto Santana aliipatia bao la tatu na la ushindi Borussia Dortmund,goli ambalo liliwafanya wachezaji na mashabiki wa Malaga wasiamini kilichotokea.

Mechi nyingine za Jumatano za hatua ya robo fainal,Juventus watawakaribisha mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich huku Barcelona wakiwa nyumbani kucheza na PSG ya Ufaransa.