Messi aipeleka Barca nusu Fainali

lionel Messi
Image caption Messi akimtoka beki wa PSG Marco Verrati

Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina anayeichezea FC Barcelona ya Uhispania Lionel Messi aligeuka shujaa wa usiku wa jumatano kwenye uwanja wa Camp Nou baada ya kuingia akitokea benchi na kubadilisha taswira ya mchezo ambao timu yake ilikuwa imefungwa bao moja kwa bila na PSG ya Ufaransa.

Messi ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Cesc Fàbregas,alionekana kuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Barcelona ambacho kilianza mchezo huo wakiwa bila ya huduma yake.

PSG ambao wametolewa kwa sheria ya magoli ya ugenini ambayo Barcelona waliyapata kwenye mchezo wa wiki iliyopita walipocheza jijini Paris na kupata sare ya 2-2. Walianza kwa kupata bao la kuongoza kwenye uwanja wa Camp Nou kupitia kwa Javier Pastore aliyemalizia pasi ya Zlatan Ibrahimovic,lakini Kunako dakika ya 71 ya mchezo Barcelona walisawazisha bao hilo kupitia kwa Pedro baada ya pasi nzuri kati ya Messi na David Villa na kufanya matokeo kuwa 1-1.

Image caption Pedro akishangilia bao lake la kusawazisha

Hadi Mchezo unamalizika, Barcelona 1-1 PSG,lakini mabingwa hao wa Ufaransa wakaondolewa kwenye michuano hiyo kwa sheria ya mabao ya ugenini ambapo katika mchezo uliopita, Barcelona walifungana mabao mawili kwa mawili na PSG huku PSG wao wakifungana na Barcelona bao moja kwa moja,hivyo Barcelona wakasonga mbele kwa kufunga idadi nyingi ya mabao ya ugenini.

Katika mchezo mwingine uliofanyika huko Turin nchini Italia, Kibibi kizee cha Turin,Juventus FC waliondolewa kwenye michuano ya Klabu bingwa barani Ulaya baada ya kichapo cha mabao mabao mawili kwa sinia na kwa jumla ya mabao matano kwa bila na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich.

Licha ya Bayern kuonekana kuimaliza shughuli mapema tangu walipoibuka na ushindi wa mabao 3-0 nyumbani wiki iliyopita,Wengi walidhani Juventus ingeutumia vyema uwanja wa nyumbani kubadilisha matokeo na kusonga mbele,lakini haikuwa hivyo.

Mario Mandzukic aliipatia bao la kwanza Bayern Munich maarufu kama The Bavarians kunako dakika ya 64 kwa kichwa saafi akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo wa Ujerumani Bastian Schweinsteiger.

Kunako dakika ya 90 ya mchezo, Claudio Pizarro alipigilia msumari wa mwisho kwenye jahazi la Juventus na kumaliza matumaini yao ya kuendelea kushiriki michuano ya kombe la klabu bingwa barani ulaya msimu huu kwa kufunga bao la pili kwa Bayern Munich.

Matokeo haya yanamaanisha ni timu nne pekee ambazo ni Real Madrid,Borussia Dortmund,Bayern Munich na Fc Barelona ndizo ambazo zitasalia kwenye michuano ya mwaka huu hatua ya nusu Fainal kabla ya fainali ambayo mwaka huu itafanyika kwenye uwanja wa Wembley jijini London mapema jumamosi ya tarehe 25 mwezi May mwaka 2013.

Droo ya kutambua nani atakuna na nani kwenye hatua ya nusu fainali inatarajia kuchezeshwa mchana wa siku ya Ijumaa ya wiki hii tarehe 12 April kwenye makao makuu ya shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA huko mjini Nyon nchini Uswis.