Je,Manchester United kutwaa Ubingwa leo?

Image caption Ferguson akiwa ameshika kombe la ligi kuu 2011

Ligi kuu ya soka nchini England itaendelea tena jumatatu ya leo kwa mchezo mmoja kati ya Manchester United watakaokuwa nyumbani kwenye uwanja wa Old Traford kuwakaribisha Aston Villa.

Mchezo huo ambao Manchester United inahitaji ipate ushindi kujihakikisha ubingwa wa 20 wa ligi kuu soka nchini England na kuweka rekodi mpya ya kuwa timu iliyochukua taji hilo mara nyingi zaidi ya Liverpool ambayo ilikuwa inashikilia rekodi ya mataji 19.

United inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kulazimishwa sare ya 2-2 na West Ham United katika mchezo wa jumatano iliyopita. Aston Villa wao watashuka uwanjani kucheza mchezo huo usiku wa leo wakiwa kwenye harakati za kuepuka kushuka daraja la ligi kuu.

United katika michezo mitano iliyopita waliyocheza wamefungwa michezo miwili,wameshinda miwili na kutoka sare mmoja huku Aston Villa katika michezo mitano iliyopita waliyocheza wamefungwa mchezo mmoja na kushinda michezo mitatu na kutoka sare moja dhidi ya Fulham.

Huu utakuwa mchezo wa 34 kwa timu zote kwenye ligi kuu soka nchini Uingereza msimu huu ambapo zitakuwa zimebakisha michezo mingine minne kumaliza ligi.

Image caption Kocha wa Manchester United,Sir Alex Ferguson akimpa maelekezo Wayne Rooney

United wanaongoza ligi wakiwa na point 81 huku wakifuatiwa na watani zao wa wajadi Manchester City ambao walifungwa hapo jana jumapili na Tottenham kwa mabao 3-1,hivyo mchezo wa leo utaweza kuwafanya United wacheze kwa uhuru zaidi na kutaka kujipa matumaini ya kuwavua rasmi ubingwa majirani zao Manchester City. Aston Villa inayofundishwa na Paul Lambert inashika nafasi ya 17 wakiwa na point 34,pointi tatu zaidi ya Wigan wenye pointi 31 wakiwa kwenye nafasi ya 18 ambayo ni kwenye kundi la timu tatu za mwisho zilizoko kwenye hatihati ya kushuka daraja.

Aston Villa katika michezo 32 iliyopita waliyocheza na Manchester United wameshinda mchezo mmoja,hiyo ilikuwa mwaka 2009 mwezi disemba pale Gabby Agbonlahor alipofunga bao la kichwa kwenye uwanja wa Old Traford. Kwa upande wa United, wao katika michezo 34 iliyopita ya ligi kuu tangu mwaka 1995 wamepoteza mara moja tu dhidi ya Villa.

Wayne Rooney anatarajia kufikisha mchezo wake wa 400 akiwa na Manchester United huku akiwa ameifungia klabu yake mabao tisa ya ligi kuu dhidi ya Aston Villa ikiwa ni rekodi nzuri kwake kuifunga timu moja idadi kubwa ya magoli,akiwa amezifunga idadi hiyo hivyo timu za Bolton, Fulham and Newcastle.

Manchester United itataka kuvunja rekodi ya Chelsea ya msimu wa 2004/05 kwa kumaliza msimu na idadi kubwa ya pointi, iwapo watashinda mechi zote zilizosalia,huenda wataifikia rekodi ya pointi 95 za Chelsea.

Mshambuliaji wa Aston Villa Christian Benteke yupo kwenye kiwango kizuri hivi sasa baada ya kufunga mabao 10 katika mechi 13 zilizopita alizoichezea Villa huku akiwa amebakisha magoli mawili ili afikie rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Dwight Yorke ya kufunga magoli mengi(17)katika msimu mmoja wa ligi kuu,ila ndiye mchezaji ambaye anaongoza kwa kuotea mipira mingi(offsides) kwenye ligi kuu msimu huu, ambapo amekwisha otea mara 49.

Mwenzake Gabby Agbonlahor yeye amebakisha goli moja ili aweze kuvunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Aston Villa, Dwight Yorke ya kufunga magoli mengi kwenye klabu hiyo. Yorke anaongoza kwa kufunga magoli 60 kwenye timu ya Aston Villa.

Nyota wa zamani wa Aston Villa ambaye kwa sasa anaichezea Manchester United Ashley Young ataikosa mechi hiyo dhidi ya timu yake ya zamani kutokana kuwa majeruhi. Mchezo huu utakuwa ni mtihani mwingine kwa mshambuliaji wa Manchester United, Robin Van Persie ambaye anasaka kiatu cha ufungaji bora wa ligi kuu kwa mara ya pili mfululizo. Hivi sasa Van Persie ana magoli 21 akiwa anashika nafasi ya pili nyuma ya Luis Suarez wa Liverpool ambaye ana magoli 23 akiongoza safu ya wafungaji kwenye ligi kuu ya Uingereza.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa majira ya saa nne za usiku kwa saa za Afrika Mashariki.