Boateng asajiliwa na Fulham

Image caption Derek Boateng

Mchezaji kiungo wa timu ya taifa ya Ghana Derek Boateng, amejiunga na klabu ya Fulham kutoka klabu ya Dnipro Ukraine.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alisajiliwa na klabu hiyo inayoshiriki katika ligi kuu ya premier kwa mkataba wa mwaka mmoja na ana nafasi ya kuuongeza kwa mwaka mwingine.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Boateng alisema ana furaha kubwa na ni fahari yake kujiunga na klabu hiyo ya Uingereza.

''Kwa miaka mingi nimekuwa nikijitahidi kufanya kila juhudi ili kucheza ligi kuu ya England, na kwa kuwa nimepata nafasi hiyo, nitajitahidi zaidi kwa manufaa ya klabu yangu'' alisema Boateng.

Kocha wa Fulham Martin Jol, amekuwa akijaribu kumsajili mchezaji huyo kwa muda mrefu, lakini azma hiyo haikutimia kutokana na matatizo kuhusiana na kandarasi ya mchezaji.

Boateng ameichezea timu ya taifa ya Ghana mara 46, na usajili huo unatarajiwa kuipa Fulham nguvu zaidi msimu ujao.

Boateng amewahi kuchezea vilabu vya Getafe ya Uhispania , Kalamata FC na Panathinaikos ya Ugiriki, Cologne ya Ujerumani na Beitar Jerusalem ya Israel.

Mchezaji huyo sasa ni wa tatu kusajiliwa na Fulham baada ya kukamilika kwa ligi kuu msimu huu.

Klabu hiyo tayari imewasajili mlinda lango Sascha Riether na Fernando Amorebieta.