Hughes huenda akateuliwa kocha wa Stoke

Image caption Mark Hughes

Klabu ya Stoke City imeanzisha mazungumzo na Mark Hughes huku ikiimarisha juhudi zake za kutafuta mrithi wa kocha aliyefutwa kazi Tony Pulis.

Klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Premier, imetangaza azma yake ya kumsajili kocha huyo ambaye hakuwa na klabu yoyote, tangu alipofutwa kazi na Queens Park Rangers Novemba mwaka uliopita.

Wasimamizi wa klbau hiyo wanahisi kuwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 49, anaweza kuiongoza klabu hiyo, ila wamekiri kuwa wanawachunguza makocha wengine.

Mazungumzo na makocha wengine huenda yakaanzishwa mwishoni mwa wiki hii.

Kocha wa Wigan Roberto Martinez, vile vile ni miongoni mwa wake wanaopigiwa upato kumrithi Pulis.

Martinez alifutwa kazi na klabu ya Stoke City siku ya Jumanne baada ya kuiongoza kwa muda wa miaka saba iliyopita.

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, Barcelona na Chelsea alianza kazi hiyo mwaka wa 1999 na timu ya Wales kabla ya kujiunga na klabu ya Blackburn mwaka wa 2004.

Baada ya kuiongoza Blackburn kwa miaka minne, alijiunga na Manchester City ambako alidumu kwa muda wa miezi kumi na minane kabla ya kufutwa kazi na mahala pake kuchukuliwa na Roberto Mancini.

Kisha alijiunga na Fulham kwa msimu mmoja kabla ya kuteuliwa kuwa kocha wa QPR, Januari mwaka wa 2012.