Kenya na Malawi zatoka sare ya 2-2

Image caption Harambee stars ya Kenya

Timu ya taifa ya soka za Malawi na Kenya zimetoka sare kwa kufungana mabao 2-2 mjini Blantyre mechi ya kufuzu kombe la dunia.

Malawi walikuwa wanaongoza mawili kwa moja lakini katika dakika ya mwisho Chimango Kayira akafunga langoni mwake mwenyewe na hivyo kupunguza sana uwezekano wa Malawi kusonga hatua inayofuata.

The Flames ndio waliotangulia kufunga dakika ya 46, bao lililofungwa na Robion Ngalande, lakini dakika sita baadaye Mohamed Jamal akaisawazishia Harambee Stars.

Katika dakika ya 81, Robert Ng'ambi alifunga bao la pili la Malawi, kabla ya Kayira kujifunga na mechi kumalizikia mawili kwa mawili.

Matokeo hayo yana maana kwamba mabingwa wa Afrika Nigeria ndio watakaofuzu hatua inayofuata kutoka kundi la F, ikiwa wataishinda Namibia mjini Windhoek, mechi inayochezwa baadaye usiku huu.

Leo inabakia mwaka mmoja kamili, kabla ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2014 kuanza nchini Brazil.